Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI KUTOA KIPAUMBELE CHA AJIRA KWA WATAALAM WA HUDUMA ZA UTENGAMAO

Posted on: July 19th, 2023

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema Serikali itatoa kipaumbele cha ajira kwa wataalam wa huduma za utengamao (Rehabilitative Services) kupitia watu waliosomea fani za Physiotherapy, Occupationa Therapy, pamoja na Audiology and Speech Language.

Waziri Ummy amesema hayo mara baada ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kutoa tangazo la fursa za masomo kwa fani hizo.

“Tuna uhaba wa wataalam hawa katika nchi yetu, hakika uwepo wao unakwenda kuwezesha watu wenye ulemavu hususani watoto kuishi maisha bora zaidi” amesema Waziri Ummy.

Amesema kuwa amefurahi kuona kozi za shahada ya kwanza za wataalamu wa Huduma za Utengamao na kukipongeza Chuo cha Muhimbili kuja na kozi hizo muhimu katika Sekta ya Afya.

"Niwatie moyo wenye sifa za kusoma kozi hii kuomba. Serikali kupitia Wizara ya Afya itatoa kipaumbele cha ajira kwa wataalam hawa" amesema Waziri Ummy.