Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI KUSHIRIKIANA NA WADAU KUTOKOMEZA MAGONJWA YASIYOPEWA KIPAUMBELE

Posted on: August 6th, 2024



Na WAF – Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendeleza juhudi za kuyakabili magonjwa yasiyopewa kipaumbele na mafanikio ya juhudi hizi yameanza kuonekana katika kuyatokomeza.

Hayo yamesemwa leo tarehe 06 Agosti 2024 na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, wakati akizindua jukwaa la kimkoa la afya, usafi wa mazingira, na kutokomeza magonjwa yasiyopewa kipaumbele. Tukio hilo liliratibiwa na Wizara ya Afya, Wizara za Kisekta na taasisi ya Helen Keller International mkoani Dodoma.

“Lengo la kukutanisha Wizara ya Elimu, Maji, kitengo cha Usafi wa Mazingira, na wadau wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ni kupeana uzoefu na kujadili mipango mbalimbali ya jinsi ya kufanya kazi pamoja ili kutokomeza magonjwa haya.” Amesema Dkt. Magembe.

Dkt. Magembe amesema jukwaa hili litasaidia kupunguza na kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ambayo yanasababishwa na ukosefu wa maji na usafi wa mazingira.

Aidha, Dkt. Magembe ameeleza kuwa uanzishwaji wa jukwaa la kimkoa la wadau wa afya, usafi wa mazingira, na kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele litatekelezwa katika ngazi ya taifa na katika mikoa minne ya Tanzania Bara ambayo ni Dodoma, Manyara, Arusha, na Rukwa jambo ambalo litapelekea robo ya mikoa yote ya Tanzania Bara kunufaika na jukwaa hilo

Hata hivyo, Meneja wa Programu wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele, Dkt. Clara Mwansasu, ameeleza kuwa Serikali imekuwa ikitekeleza afua za kutokomeza magonjwa hayo ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi, kumezesha dawa kwa walioathirika, na kufanya kampeni za uhamasishaji baada ya kufanya tathmini ya kina.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Helen Keller, Dkt. Joyce Lyamuya, amewataka wadau wa sekta ya afya kuungana kwa pamoja na kushirikiana na Serikali ili kusaidia kutokomeza magonjwa yasiyopewa kipaumbele.