Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI KUSHIRIKIANA NA UBONGO LEARNING KUFIKISHA ELIMU YA AFYA KWA WATOTO

Posted on: March 18th, 2024


Na. WAF Dodoma


Wizara ya Afya kupitia sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma kwa kushirikiana na shirika la Ubongo Learning imejipanga kuendelea kufikisha elimu ya Afya kwa watoto wenye miaka 3 mpaka 14 kwa njia ya katuni 


Hayo yamesemwa na Afisa Program kutoka Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma Bw. James Mhilu katika kikao kazi cha kuandaa jumbe za Afya zitakazo tumika katika msimu wa tano wa katuni ya 'Akili and Me' kimechofanyika leo Jijini Dodoma


Bw. Mhilu amesema, wote ni mashuhuda tunapambana na magonjwa yasiyoambukiza, matumizi sahihi ya vyoo, usafi wa mazingira na usafi wa mtu binafsi ni kwa sababu jamii kubwa kwa sehemu iliyopo ilikosa haya mafunzo na malezi katika nyakati zao za utotoni.


"Kama wizara ya Afya tumeona tutumie fursa hii kwa kushirikiana na wenzetu wa Ubongo kwa ajili ya kufikisha elimu hizi kwa watoto wenye umri kati ya miaka 3 mpaka 14 ili kuwafundisha katika maeneo mbalimbali muhimu ya Afya kwa sababu tuna amini kwamba ukitaka kutengeneza kizazi cha watu wanao wajibika na afya zao ipasavyo ni kuanza na watoto " Amesema.


Pia Bw. Mhilu amesema kuendelea kutumia katuni hizi kuwafundisha watoto mtindo bora wa maisha itasaidia sana kuwa na kizazi ambacho kinajua nini kifanye na nini kisifanye na itaipunguzia Serikali mzigo mkubwa wa kuhudumia wagonjwa wanao ugua magonjwa ambayo yangeweza kutibika kwa kubadili mtindo wa maisha.


"Leo tuna mzigo mkubwa wa matatizo ya magonjwa yasiyoambukiza kwa sababu maisha ambayo tunayo ishi ni matokeo ya yale tuliyofundishwa utotoni, mtu anaona kula vyakula ambavyo wataalau wa afya hawavishauri ndio ufahari"amesema.


Kwa upande wake Afisa Utafiti na Mawasiliano Kutoka Ubongo Learning Bi. Veronica Kilala Amesema ubongo Kids itaendelea kutumia Elimu burudani kwa kutumia michoro ili kufikisha ujumbe kwa watoto.


"Tutatumia mada mbalimbali zinazo husiana na Afya ikiwemo masuala ya Lishe, matumizi sahihi ya vyoo pamoja na mada mbalimbali ambazo zinawalenga watoto ili kuweza kufikisha elimu sahihi kwa kutumia majukwaa mbalimbali tuliyonayo" Amesema