Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA UKATILI WA KIJINSIA.

Posted on: December 18th, 2024

Na WAF - DSM

Serikali imedhamiria kushughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto nchini, kwa kuzidi kuimarisha mifumo, miundombinu na uratibu katika vituo vya kutolea huduma za wahanga ukatili wa kijinsia na  ukatili dhidi ya watoto ili kuwajengea uwezo watoa huduma wanaotoa huduma hizo.

Hayo yamebainishwa Desemba 17, 2024 na Mkurugenzi wa Huduma za kinga Dkt. Ntuli Kapologwe wakati akifungua mkutano wa uenezaji wa matokeo ya utafiti wa kupunguza ukatili wa wapenzi kati ya wanawake wajawazito katika kambi ya Nyarugusu unaoendelea Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Ntuli amesema Utafiti unaonyesha  maeneo yenye ukatili mwingi wa kijinsia kuna matumizi hafifu ya huduma za afya ya uzazi, jambo linaloonyesha kwamba ukatili wa kijinsia unachangia uzoroteshaji wa utumiaji wa huduma za afya ya uzazi.

“Vyanzo vikuu vya  ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya mtoto ni pamoja na mila na desturi potofu, umasikini,  kushuhudia au kuwa na historia ya kukatiliwa mara nyingi, kutoheshimu haki za binadamu, Ugonjwa wa akili, kutokuwa na usawa wa Kijinsia,” amesema Dkt. Ntuli.

Dkt. Ntulli pia ameasa wataalam hao kuangalia mbinu za nasaha zilizopo kulinganisha na mbinu za nasaha zilizotumika katika utafiti huu ili kuona kufanya maboresho kwa kile kimekosekana kulingana na  rasilimali na mazingira ya nchi.

Ameongeza kuwa Serikali inashukuru  na kutambua, mchango wa Shirika la Afya Duniani  (WHO) kwa kuendelea na tafiti mbalimbali zinazohusiana na afya na ustawi wa jamii nchini na  duniani kote.

“Natoa wito kwa wadau wengine kuendelea kufanya tafiti hizi, katika eneo hili hasa kwa mambo ambayo hayana majibu ya kutosha kuhusu mambo mbalimbali yanayohusiana na ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto, ili kupata ufumbuzi, pia kupanua eneo la utafiti huu, kwa maeneo mengine ya nchi yetu ili kuwe na uwakilishi toshelevu wa matokeo,” amesema Dkt. Ntuli.