Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI KUFUNGUA TAWI LA JKCI CHATO

Posted on: May 13th, 2024

Serikali imepanga kufungua tawi la Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Kanda ya Ziwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (JKCI- Chato) iliyopo mkoani Geita.

Hayo yamesemwa Tarehe 13 Mei, 2024 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2024/25.

Katika kutekeleza hilo Wizara ya Afya moja ya vipaumbele vyake kwa mwaka wa fedha wa 2024/25 ni  kuwekeza katika vifaa tiba vitakavyowezesha utoaji wa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi ikiwemo ununuzi wa mitambo ya kupima na kutibu moyo bila kufungua kifua (Cathlab) miwili kwaajili ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya na Chato.

Waziri Ummy alisema huduma za ubingwa na ubingwa bobezi  zinapatikana kwa gharama nafuu nchini na hivyo kuvutia wagonjwa kutoka nje ya nchi (Tiba Utalii) ambapo wagonjwa kutoka nje ya nchi wameongezeka kutoka 5,705 mwaka 2022 hadi 7,843 mwaka 2024.

“Katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi katika Hospitali ngazi ya Taifa, Kanda, Maalum na hospitali za Mikoa, Aidha, kutokana na uwekezaji wa kimkakati uliofanywa na Serikali wa kuimarisha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi”.
“Huduma mpya 16 za ubingwa bobezi zilianzishwa nchini zikiwemo za upasuaji mdogo wa moyo kwa kubadilisha Valvu ya mshipa mkubwa wa damu bila kufungua kifua (Transcatheter Aortic Valve Implamentation - TAVI), kufungua mishipa ya miguuni iliyoziba (Endovascular Procedure ) na  kuweka stent kwenye mishipa mikubwa ya damu iliyopasuka”, alisema Mhe. Ummy.

Katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi nchini kwa kutumia wataalam wa ndani, kiasi cha Shilingi 5,000,000,000 kimetolewa kwaajili ya kugharamia matibabu kwa wagonjwa wasio na uwezo wa matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi jumla ya wagonjwa 237. Huduma hizo zimetolewa katika hospitali za Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ilihudumia wagonjwa 100 ambapo kati yao wagonjwa 50 walipatiwa huduma za Valvular Replacement surgery na wagonjwa 50 walipatiwa huduma za Implantable cardiac devices.