Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI KUENDELEZA MAPINDUZI SEKTA YA AFYA

Posted on: July 14th, 2024



Na WAF - KATAVI 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inaendeleza jitihada za kusogeza huduma za Afya karibu na wananchi kwa kuboresha miundombinu ya kutolea huduma kuanzia ngazi ya msingi ili kuimarisha huduma za Afya nchini.


Rais Samia amesema hayo Julai 14, 2024 Mkoani Katavi alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo ili kujionea hali ya utoaji wa huduma na maendeleo ya miradi ya ujenzi.



Rais Samia amesema Serikali tayari imeshapeleka fedha za ujenzi wa awamu ya pili ya Hospitali hiyo pia inatazamiwa kuongeza vifaa vya huduma za kibingwa.


“Hizi ni jitihada za Serikali kusogeza huduma za afya karibu sana na wananchi, ambapo ndani ya mkoa huu wa Katavi tumefanya kazi ya kuongeza vituo vya Afya, Hospitali za wilaya, kata hadi kule chini kwenye zahanati. Kwahiyo lengo ni kusogeza huduma za Afya karibu na Wananchi". Amesema Rais Samia na kuongeza.


"Hospitali kama hizi tulizoea kuzisikia huko Dar es salaam Mwanza na Arusha lakini leo hospitali hii ipo Katavi, nimekwenda kuangalia Wodi ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati nimeona huduma iliyopo pale ni sawa na huduma iliyopo Dar es salaam Wodi ya watoto ambao hawakutimiza miezi 9, Mashine za kisasa na wataalamu wapo”. Amesisitiza Rais Samia.


Rais Samia ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha Hospitali hiyo kwa ujenzi wa awamu ya pili na ya tatu kwa kujenga majengo mengine zaidi ya kutolea huduma.



“Kinachotumika sasa ni awamu ya kwanza ya Ujenzi wa hospitali hii lakini kuna awamu ya pili na awamu ya tatu kama inavyooneshwa kwenye ramani, fedha za ujenzi wa awamu ya pili tayari zimeshafika kwahiyo Hospitali hii itaendeleza ujenzi kujenga majengo mawili zaidi ya kutolea huduma na tutaendeleza ikamilike kama ilivyo kusudiwa kwenye Ramani”. Amefafanua Rais Samia.


Rais Samia pia ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi wa Mkoa wa Katavi na Tanzania kwa ujumla kujiunga na Mfuko wa bima ya Afya kwa wote. 


“Niwaombe sana watakapokuja Mfuko wa bima kwa Afya, Kila Mwananchi anunue bima yake na familia yake mara moja kwa mwaka unatibiwa na familia yako mwaka mzima. Tusaidieni kununua Bima za Afya ili tuweze kujenga na kutoa huduma zaidi katika mahospitali ya aina hii lakini hata hospitali zetu za mikoa na Wilaya na zile za kata kule chini, niwaombe sana twendeni tukaunge kono huduma hizi za Bima ya Afya ili Afya ya Mtanzania iweze kuimarika na kusambaa kwa kila mtanzania aweze kunufaika". Amesema Rais Samia.


MWISHO