SERIKALI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA
Posted on: September 26th, 2024
Na, WAF Arusha
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Bw. Ismail Rumatila amesema Serikali inashirikiana na Sekta Binafsi na Mashirika ya Dini katika utoaji wa huduma za Afya kwa Wananchi ikiwa ni Sera ya Afya ya 2007 katika kuboresha huduma za afya katika jamii.
Bw. Rumatila ameyasema hayo leo Septemba 25, 2024 katika jubilee ya miaka 60 ya Hospitali ya Wasso iliyofanyika katika Wilaya ya Ngorongoro Jijini Arusha.
“Serikali inashirikiana na Sekta Binafsi na Mashirika ya Dini katika utoaji wa huduma za Afya kwa Wananchi ikiwa ni Sera ya Afya ya 2007 sambamba na Mwongozo wa Ubia kati ya Sekta Binafsi na Umma, hivyo Wizara yangu itahakikisha inatekeleza kwa umakini na ufanisi”. Amesema Bw. Rumatila
Aidha Bw. Rumatila ameupongeza uongozi kwa Mikakati iliyowekwa juu ya uboreshaji wa huduma za afya pamoja na ushirikiano uliopo kati ya Wafadhili mbalimbali kwa ajili ya kuboreha huduma za Afya ikiwa ni pamoja na kuongeza vifaa vya uchunguzi na upasuaji, kuendelea kusomesha wataalam katika kada mbalimbali za Afya, kuwa na nishati ya uhakika, kuwatumia wataalam wa nje ya nchi kubadilishana maarifa na ujuzi na mifumo thabiti ya TEHAMA.
Bw. Rumatila amesema mkakati wa Hospitali kuwa wa kuanzisha Chuo cha Uuguzi na Ukunga ambacho kitasaidia kuzalisha wataalam wa Afya pamoja na kuweza kukabiliana na upungufu mkubwa wa watumishi wa Afya wa kada hiyo pia ni fursa kwa vijana kujipatia ajira katika chuo hicho.
Kwa upande wake Mhashamu Baba Askofu Mkuu Isaack Amani, amewataka watumishi wa afya katika Hospitali hiyo kuwa waadilifu na kufanya kazi kwa weledi ili kuendelea kunusuru maisha ya watanzania ambao wanakumbwa na changamoto za kiafya.