Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI KUBORESHA HUDUMA ZA UTENGAMAO KWENYE HOSPITALI ZA MIKOA KUFIKIA 2026

Posted on: October 6th, 2024

Na, WAF-Mwanza

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amesema kuwa serikali imejipanga kuhakikisha hospitali zote za mikoa nchini zinatoa huduma za utengamao ifikapo mwaka 2026, kama sehemu ya juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuboresha huduma za afya.

Akizungumza kwenye Kongamano la 5 la Kisayansi na Mkutano wa Chama cha Wataalamu wa Viungo na Vifaa Tiba Saidizi Tanzania (APOT) uliofanyika jijini Mwanza, Dkt. Mollel amesema huduma za utengamao zimewekwa kuwa moja ya vipaumbele vya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

“Serikali imetenga shilingi bilioni 5 kwa ajili ya kuboresha huduma hizi, ambapo bilioni 3 zitatumika kwenye miundombinu na bilioni 2 kwa ununuzi wa vifaa vya kisasa pia, teknolojia ya juu zaidi itatumika katika huduma hizi, huku mkoa wa Tabora ukipewa kipaumbele” amesema Dkt. Mollel.

Dkt. Mollel pia amewataka wataalamu wa utengamao kuongeza ubunifu katika kazi zao, hususan katika kutengeneza vifaa tiba bandia ili kusaidia kuboresha huduma na kupunguza changamoto zinazowakabili watu wenye uhitaji.

Aidha, amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuunga mkono sekta binafsi katika juhudi zao za kuboresha huduma za afya, akiwataka kutoa taarifa za changamoto wanazokumbana nazo kwa mamlaka husika ili kupata ufumbuzi wa haraka.

Katika mkutano huo, Naibu Waziri amekabidhi vifaa vya utengamao kwa watu 35 ambao wamenufaika na udhamini wa SwissAbility, shirika linalojihusisha na kusaidia maendeleo katika sekta ya afya ambapo vifaa hivyo vimetolewa ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za kuimarisha upatikanaji wa huduma za utengamao kwa watu wenye uhitaji nchini.

Kongamano hilo la kisayansi limeleta pamoja wataalamu wa afya kutoka sehemu mbalimbali za nchi, ambapo walipata fursa ya kubadilishana mawazo na kujadili mbinu bora za kuboresha huduma za afya, hususan huduma za utengamao ambazo ni muhimu kwa watu wenye ulemavu au mahitaji maalum ya viungo.