Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI INATAKA KUONA WANANCHI WANAPATA HUDUMA BORA

Posted on: April 14th, 2023

Na. WAF - Dodoma

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya afya inataka kuona wananchi wanapata huduma bora katika Hospital za Rufaa za Kanda, Mikoa hadi Zahanati.

Dkt. Shekalaghe ameyasema hayo leo wakati akifunga Mkutano wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Sekta ya Afya uliofanyika kwa siku mbili Jijini Dodoma.

“Serikali imejenga majengo makubwa mazuri na imenunua vifaa tiba lengo likiwa ni kumuondolea usumbufu mgonjwa na afurahie kupata huduma bora ili aipende Serikali yake,” amesema Dkt. Shekalaghe

Kuhusu suala la uongozi, Dkt. Shekalaghe amesema kuna kitu kinaitwa Humility ambacho kinabeba mambo matatu ikiwemo kuelewa nafasi ya uongozi kuwa ni bahati, mafanikio ya kiongozi yanatokana na wengine pamoja na kutambua kuwa kila mtu anafanya makosa.

“Ukishakuwa kiongozi lazima uwaambie kwanza watu unaowaongoza kuwa unataka nini kisha kama hawatafata kile ambacho unataka ndio uchukue hatua pale inapobidi,” amesema Dkt. Shekalaghe

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe amesema ili kuboresha huduma za afya lazima pia kufuatilia na kusimamia rasilimali zote zilizomzunguka mgonjwa.

“Kuboresha huduma ni pamoja na kusimamia magari ya wagonjwa, tuweke vitanda bora sio unamuweka mgonjwa kwenye godoro ambalo lina kunguni hii sio sawa,” amesema Dkt. Magembe

Pia, Dkt. Magembe amesema watumishi wanatakiwa kujuana, kuheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana hapo ndio tutaweza kumuonesha upendo mgonjwa na kumpa huduma bora.

Nae, Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amewataka watumishi wote katika sekta ya afya kusimamia miongozo ya ugawaji dawa ili kuepuka kumwandikia mgonjwa dawa ambazo hazipo au zimekwisha muda wake.

Mwisho, katika Mkutano huo wa Baraka Kuu la Wafanyakazi wameazimia kufanyia kazi maelekezo ya viongozi, kutekeleza mkakati harakishi wa kuboresha huduma, kufanyia kazi maoni yote yaliyotolewa na Tughe pamoja na wajumbe wa Baraza hilo pamoja na watumishi kufuata maelekezo ya Serikali.