SERIKALI IMENUNUA NA KUSIMIKA VITI VYA KUTOLEA HUDUMA ZA KINYWA NA MENO 150
Posted on: May 16th, 2024UTEKELEZAJI WA BAJETI YA WIZARA YA AFYA 2023/24
Na WAF - Dodoma
Wizara ya Afya imeimarisha Huduma za Afya ya Kinywa na Meno hapa nchini katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024 Wizara imenunua na kusimika viti vya kutolea huduma za kinywa na meno 150 vilivyosambazwa kwenye Hospitali za Rufaa za Mikoa Minne pamoja na vituo vya Halmashauri 142.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo Bungeni Mei 13, 2024 akiwa anawasilisha hotuba yake ya bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2024/25 akielezea utekelezaji wa majukumu ya Wizara katika utoaji wa huduma za Kinga nchini.
"Wizara ilinunua na kusambaza X-Ray za meno 103 kwenye Halmashauri 87 nchini, ununuzi wa mashine kubwa tatu (3) za kisasa zenye teknolojia ya hali ya juu ya kutambua magonjwa ya kinywa na meno kwa mfumo wa ki-Radiolojia aina ya '3D - Dental Cone Beam Computerized Tomography (CBCT)'." Amesema Waziri Ummy
Amesema, mashine hizo zimefungwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali ya Rufaa Kanda Mbeya pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mount Meru ambapo Tanzania ni nchi pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kununua vifaa hivyo katika Hospitali za umma.
Aidha, Waziri Ummy amesema katika kipindi hiki, jumla ya wagonjwa laki 592,732 wa kinywa na meno walihudhuria kwenye vituo vya kutolea huduma hizo.
"Magonjwa ya kinywa na meno yaliyoongoza ni kuoza meno, wagonjwa 395,685 sawa na 66.8%, magonjwa ya fizi wagonjwa 57,091, sawa na 9.6%, Jipu la jino wagonjwa 15,633, sawa na 2.6% pamoja na mpangilio mbaya wa meno 13,734 sawa na 2.3%." Amesema Waziri Ummy
Waziri Ummy amefafanua kwamba wagonjwa laki 144,607 ambao ni sawa na asilimia 36.5 waliooza meno walipata matibabu ya kuziba meno, wagonjwa 251,078 saww na asilimia 63.5 waling’olewa meno.
"Naomba kutoa wito kwa watanzania wote kuwahi kufika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ya meno mapema pindi wanapopata shida ya meno ili kuepuka kung’olewa meno kwa kuwa magonjwa ya meno yanatibika, ’’dawa ya jino siyo kung’oa”. Amesisitiza Waziri Ummy