SERIKALI ILITUMA TIMU YA WATAALAMU KUCHUNGUZA MARBURG KAGERA-DKT. SAMIA
Posted on: January 20th, 2025
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema mtu mmoja amekutwa na maambukizi ya virusi vya Marburg (MVD) katika Wilaya ya Biharamuro mkoani Kagera.
Taarifa hiyo inakuja siku sita tangu Shirika la Afya Duniani (WHO) liweke wazi kuhusu watu wanane kufariki dunia kutokana na ugonjwa unaoshukiwa kuwa wa virusi vya Marburg mkoani humo.
Rais Samia ameyasema hayo leo Jumatatu, Januari 20, 2025 alipozungumza na waandishi wa habari mkoani Dodoma, akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus.
Rais Samia amesema Serikali ilituma timu ya wataalamu Januari 11 mwaka huu mkoani humo na kufanya uchunguzi kuhusu ugonjwa huo na katika sampuli zilizochukuliwa ni mgonjwa mmoja pekee aliyekutwa na maambukizi hayo.
Baadhi ya dalili ya Virusi vya Marburg ni pamoja na Homa kali, Kuumwa Kichwa, Kutapika au kutapika damu, kuharisha au kuhara damu, kutokwa na damu Sehemu mbalimbali za mwili .
Aidha, jinsi ya kujikinga na Marburg ni pamoja na kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni mara kwa mara, kuepuka kugusa au kuosha maiti ya mtu aliyefariki na ugonjwa wa Marburg, kuepuka kula au kugusa mizoga, na kuepuka kusalimiana kwa kushikana mikono.