SERIKALI, HELEN KELLER INT'L WASHIRIKIANA KUFIKISHA HUDUMA ZA KIBINGWA KARIBU NA WANANCHI
Posted on: August 14th, 2024
Na WAF - Songwe
Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya afya kuboresha huduma bora za afya nchini, hususani huduma za kibingwa, kwa kuhakikisha huduma hizo zinasogezwa karibu na wananchi ndani ya kilomita tano.
Hayo yameelezwa na Dkt. Ama Kasangala kutoka Wizara ya Afya kupitia kitengo cha magonjwa yasiyoambukizwa, tarehe 9 Agosti, 2024, wakati wa kambi ya huduma za matibabu ya upasuaji wa mtoto wa jicho iliyofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Wilaya ya Songwe. Kambi hiyo ilifadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali la Helen Keller International.
Dkt. Kasangala amesema zaidi ya wagonjwa 450 wamepatiwa huduma ya matibabu ya upasuaji wa mtoto wa jicho bure, hali ambayo imepunguza rufaa za wagonjwa hao kwenda hospitali za kanda.
“Awali, wananchi hawa walihitajika kusafiri hadi Hospitali ya Kanda, Mbeya kupata huduma hii, lakini kupitia kambi hii, wote wamepatiwa huduma hapa Songwe bila malipo yoyote,” alisema Dkt. Kasangala.
Amewashukuru viongozi wa wilaya ya Songwe kwa ushirikiano waliotoa katika kipindi chote cha kambi hiyo na kulipongeza shirika la Helen Keller International kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali za kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.
Kwa upande wake, Meneja Mradi kutoka shirika la Helen Keller International, Athuman Tawakal, amesema jumla ya wagonjwa 700 wamefanikiwa kupatiwa huduma ya matibabu ya upasuaji wa mtoto wa jicho katika Wilaya ya Songwe.
“Hii ni awamu ya pili ya kambi ya upasuaji wa mtoto wa jicho kufanyika hapa Songwe, ambapo awali tuliwahudumia wagonjwa 300 na sasa ni 400, na lengo ni kufikia wagonjwa 700. Matibabu haya yote ni bure, na tunawafuata wagonjwa katika maeneo yao kwa kutumia gari na kuwapatia chakula pamoja na ndugu waliowasindikiza hospitalini.” Amesema Bw. Tawakal.
Bw. Tawakal ameongeza kuwa lengo la shirika hilo ni kuunga mkono jitihada za serikali katika kuhakikisha huduma ya upasuaji wa macho inawafikia wananchi wote wenye uhitaji. Amefafanua kuwa baada ya kutoka Mkoa wa Songwe, huduma hiyo pia itatolewa katika Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe, Kyela mkoani Mbeya, na wilaya ya Chunya kwa mara ya pili.