Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI, AMREF KUENDELEA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA AFYA KWA JAMII

Posted on: December 13th, 2024

Na Waf Dodoma

Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na Amref kutekeleza miradi mbalimbali yenye lengo la kuiwezesha jamii katika kukabiliana na changamoto za afya kwenye eneo la huduma kamilifu za kinga, matunzo na tiba ya VVU ili kuharakisha kufikiwa kwa malengo ya sasa ya 95-95-95 kwa kudhibiti janga la VVU ifikapo 2030.

Hayo yamesemwa leo tarehe 12 Desemba, 2024 mkoani Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu wakati akifungua kikao kati ya wataalam wa Wizara ya afya na Amref cha kujadili mradi wa Afya Thabiti unaotekelezwa chini ya ufadhili wa
CDC/PEPFAR katika mikoa ya Mara na Simiyu.

Dkt. Jingu amesema ajenda kubwa iliyopo chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha huduma za afya zinamfikia kila mtu nchini katika ubora wa hali ya juu, na ili lengo hilo liweze kutimia inahitaji nguvu ya pamoja kati ya Serikali na wadau ikiwemo Amref.

"Tunakubaliana kwamba popote kwenye changamoto za afya kama milipuko ya magonjwa, kwa kiwango kikubwa inachangiwa na viashiria vya kijamii, hivyo jambo hilo inabidi tuendelee kulitilia mkazo ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri ya watu wote kupata huduma za afya," amesema Dkt. Jingu.

Pia amesema baada ya kufanya tathmini ya majadiliano hayo itasaidia katika utekelezaji wa miradi, wote tutakuwa na uelewa wa pamoja na kujua miradi hii lengo lake ni nini changamoto ziko wapi na tuzikabili vipi.

Dkt. Jingu pia ametoa wito kwa wadau hao kuhakikisha wanahakikisha wadau wengine na sekta binafsi kuona afua zinazofanyika katika mradi huo zina faida na kwao pia.

"Wadau wengine wakiona afua zilizopo zitawasaidia na wao pengine kupunguza gharama ama kuzalisha zaidi, hawataona shida kuchangia pale panapohitajika," amesema Dkt. Jingu.

Aidha Dkt Jingu ameipongeza Amref kwa kuwa mstari wa mbele kushirikiana na wizara katika kutatua changamoto mbalimbali za kiafya katika jamii.

"Mmekuwa wadau muhimu katika kuwajengea uwezo watoa huduma za kukabiliana na changamoto za afya kwani hiyo ni nyenzo muhimu katika kufikia huduma za afya kwa wote," amesema Dkt. Jingu.