SEKTA BINAFSI MSINGI WA MAENDELEO ENDELEVU NCHINI TANZANIA
Posted on: December 14th, 2024
Na, WAF-Dodoma
Uwepo wa Sekta binafsi nchini umetajwa kuwa muhimili muhimu wa maendeleo ya taifa, huku ushirikiano wa karibu kati ya sekta hizo na Serikali umewezesha kufanikisha ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel alipomuwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango kwenye mahafali ya nane ya Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Decca, leo Desemba 13, 2024 kilichopo Nala, Dodoma.
Dkt. Mollel amesema sekta binafsi inapaswa kuonekana kama injini ya uchumi wa taifa, huku akiwataka wataalamu na wahitimu wa vyuo vikuu kushirikiana kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha huduma nchini.
"Kwa muda mrefu tumekuwa tukitegemea Serikali kama chanzo kikuu cha maendeleo, lakini sasa ni wakati wa kubadilisha mtazamo. Sekta binafsi ndiyo injini ya uchumi wa dunia. Tanzania inahitaji vijana wabunifu, wenye maono na walio tayari kujenga mifumo ya kiuchumi inayojitegemea kupitia sekta binafsi," amesema Dkt. Mollel.
Aidha, Dkt. Mollel amewahamasisha wahitimu kuonyesha ubunifu na uvumbuzi wanapoingia katika sekta ya afya, akibainisha kuwa changamoto zilizopo ni fursa za kuleta mabadiliko ambapo amesema tunahitaji wataalamu wa afya watakaotumia maarifa yao kubuni mbinu mpya za kuboresha huduma za afya kwa kutumia teknolojia na uvumbuzi.
Kwa upande wake Waziri Mkuu mstaafu Mhe. Mizengo Pinda amewataka wanafunzi hao kuendeleza elimu na badala yake wasiishie kwenye astashahada na stashahada kwakua zama za sasa zina uhitaji wa elimu ya juu tofauti na miaka ya nyuma.
Mahafali hayo ya nane ya chuo hicho yalizinduliwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Mollel akimuwakilisha Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ambaye alialikwa kuwa mgeni rasmi.