Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SARATANI TISHIO ULIMWENGUNI, NAFASI YA PILI KUSABABISHA VIFO

Posted on: June 9th, 2024



Na WAF - Marekani

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema ugonjwa wa Saratani unashika nafasi ya pili kwa kusababisha vifo ulimwenguni, huku wanawake wakiwa waathirika zaidi kwa saratani ya shingo ya mlango wa kizazi na matiti nchini Tanzania imefahamika.

Dkt. Mollel amesema hayo Juni 8, 2024 akimuwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu katika Mkutano wa Kilele cha Kichocheo cha Afya Duniani uliofanyika nchini Marekani.

Dkt. Mollel amesema zaidi ya visa 40,000 vya saratani hugundulika kila mwaka na takribani watu 30,000 hufa kutokana na ugonjwa huo kwa mwaka.

“Kiwango cha saratani na vifo kutokana na ugonjwa huo bado kinabaki kuwa juu kutokana na uwasilishaji wa wagonjwa katika hatua za mwisho za ugonjwa huo katika vituo vya afya. Ongezeko la ugonjwa wa Saratani haukubaliki hivyo inatupasa tuje na kusisitiza hitaji la dharura la mikakati kamili ya kuzuia na kupambana na saratani”. Amesema Dkt. Mollel.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea na jitihada za kuimarisha huduma za Afya ikiwepo kuhakikisha upatikanaji wa dawa zote za kupambana na saratani zinapatikana na kuongeza vifaa tiba na wataalam wa kutosha.

“Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia imeimarisha upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa katika hospitali zote nchini na imeanzisha mpango maalum wa ufadhili wa masomo kwa watumishi wa sekta ya afya ikiwa na pamoja kusomesha wataalam wa Oncologist, radiologia, radiotherapist kama hatua muhimu ili kuboresha huduma za saratani”. Ameeleza Dkt. Mollel

“Mradi huu wa TRACCE utarahisisha udhibiti wa saratani katika kiwango bora ili kupunguza rufaa ya wagonjwa nje ya nchi. Kituo cha ubora nchini Tanzania kitaipunguzia Serikali mzigo kwa kuzingatia ukaribu pia utasaidia nchi jirani kuwapa rufaa wagonjwa wao nchini Tanzania”. Amesema Dkt. Mollel.

MWISHO