Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

RUVUMA YAPOKEA BIL 22.9 KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA

Posted on: July 23rd, 2023

NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amebainisha kuwa Mkoa wa Ruvuma umepokea kiasi cha Shilingi Bilioni 22.9 kwaajili ya kuboresha huduma za afya ikiwemo eneo la ununuzi wa dawa na vifaa tiba pamoja na ujenzi wa miundombinu mbalimbali ili kuondoa changamoto ya huduma kwa wananchi.

Dkt. Mollel amesema hayo leo Julai 23 alipokuwa katika ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ya kukagua miradi mbalimbali katika Mkoa wa Ruvuma ikiwemo mradi wa jengo la huduma za Mionzi.

"Mhe. Makamu wa Rais kwanza nianze kumshukuru Mhe. Rais wetu na wewe kwa kuupa Mkoa wa Ruvuma shilingi Bilioni 22.9 kwa ajili ya Sekta ya Afya ambayo Mbunge wenu mjanja wa jimbo la Mbinga amewavutia shilingi Bilioni 1.2 kwaajili ya kuboresha huduma za Afya kwaajili ya wananchi wa Wilaya yenu." Ameeleza.

Amesema, Wakati Serikali ya awamu ya sita inaingia madarakani ni hospitali mbili tu zilikuwa na huduma za CT-SCAN nchi nzima, na kusisitiza mpaka sasa hospitali zote za Rufaa za Mikoa zimesimikwa na kuanza kutoa huduma za CT-SCAN na kuokoa fedha nyingi zilizokuwa zikitumika kufuata huduma hizo katika mikoa ya Jirani.

Aidha, Dkt. Mollel amesema, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma ni moja kati ya hospitali iliyopata bahati ya kuwa katika mpango wa kupata huduma za MRI ambazo hupatikani katika hospitali za kanda na hospitali ya taifa.

Sambamba na hilo, Dkt. Mollel amesema tayari Wizara ya Afya imeanza kuwasiliana na Wizara ya Habari na Teknolojia ya Mawasiliano ili kufunga Mkongo wa taifa utaosaidia Mawasiliano katika huduma za X-ray kutoka hospitali ya Mkoa wa Ruvuma kwenda Hospitali ya Muhimbili ili kurahisisha upatikanaji huduma kwa haraka na kwa ubora