RRH. SIMAMIENI VITUO VILIVYO CHINI YENU
Posted on: July 4th, 2024
Na WAF – Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara ya Tiba Dkt. Hemed Nyembea amesema mifumo ya Afya nchini inazitambua Hopitali za rufaa za mikoa kuwa kiunganishi kati ya huduma za afya ngazi ya msingi kwa kuwa na jukumu la kuhudumia vituo vya afya ngazi zote za mkoa.
Ameyasema hayo leo Julai 4, 2024 jijini Dodoma wakati wa zoezi la ukaguzi shirikishi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ambapo kamati ya ukaguzi kutoka wizara ya afya ilitembelea na kukagua idara hospitalini hapo.
Amesema dhana hiyo inaipa jukumu hospitali za mikoa kuhudumia vituo vya afya ngazi za chini ili vituo hivyo viwe na uwezo wa kuhudumia wagonjwa kwa kiwango chao na kupunguza rufani za wagonjwa kwa hospitali za mikoa.
“Hospitali ya rufaa ya mkoa inatakiwa kufanya huduma za mkoba (outreach) kwenye Halmashauri za Mkoa, ambapo nimeambiwa hapa zinafanyika hivyo ninahimiza kuendelea kupanga ratiba vizuri ili kila idara iweze kutembelea kila Halmashauri ya mkoa kwa kufuata taarifa juu ya changamoto wanalizonazo na kutatua changamoto hizo,”. Amesema Dkt. Nyembea
Dkt. Nyembea ameitaka menejimenti ya Hospitali hiyo kuelewa vizuri dhana ya ubora wa huduma kwa kuifahamu misingi yake na kuiwakilisha kwa kila mtumishi wa kila idara na kuongeza kuwa suala la huduma kwa mteja linapaswa kubeba na kuchukuliwa kwa uzito na kila mtumishi wa sekta ya afya.
“Malalamiko mengi yanayokuja yanaonyesha kuwa suala la mawasiliano limekuwa ni shida ambapo mawasiliano ni sehemu muhimu ya kumhudumia mgonjwa, tunafahamu wote na tumesoma kuwa mgonjwa kwenye matibabu ndio kiini cha ugonjwa alio nao na kufanya maamuzi, tujitahidi sana kuboresha huduma kwa mteja “. Ameeleza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dkt. Ernest Ibenzi amesema Hospitali hiyo imeendelea kuunga mkono juhudu za Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuhakikisha watanzania wanapata huduma bora na kuwafikia walipo kwa kupeleka Madaktari bingwa maeneo mbali mbali ya nchi kwa lengo la kusaidia utoaji wa huduma sambamba na kusambaza vifaa tiba kwa wagonjwa waliovunjika mifupa mirefu.
“Juzi tulipeleka madaktari bingwa 12 katika kambi ya matibabu mkoani Arusha kwa ajili ya kusaidia kutoa huduma na pia hopsitali tunasambaza vifaa tiba vya kutibu wagonjwa waliovunjika mifupa mirefu ambapo tayari tushapeleka Hospitali ya Mt. Meru, Njombe, Shinyanga na hivi sasa tunaelekea Morogoro lengo likiwa ni huduma hizi za mifupa zifanyike katika hospitali zote za mikoa”
Aidha , Dkt. Ibenzi ameshukuru kwa ujio wa Kamati hiyo ya ukaguzi kutoka Wizara ya Afya kwa sababu imewezesha kuibua changamoto mpya na kuahidi kuzibeba na kuzifanyia kazi mara moja.
MWISHO.