RAS NJOMBE, AWASIHI WANANCHI KUJITOKEZA KUPATA HUDUMA ZA KIBINGWA NA BOBEZI
Posted on: May 26th, 2025
Na WAF, Njombe
Madaktari Bingwa na Bobezi wa Rais Samia wameanza kutoa huduma za kibingwa na bobezi katika halmashauri sita za Mkoa wa Njombe huku Katibu Tawala wa Mkoa huo, Bi.Judica Omari akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupatiwa huduma hizo.
Madakatari hao wa magonjwa ya ndani, wanawake, Watoto wachanga, upasuaji, koo, masikio na pua watatoa huduma kuanzia leo Mei 26-31, 2025 ambapo wakazi wa maeneo hayo watapata huduma mbalimbali kutoka kwa wataalam hao ikiwa ni sehemu ya kusogeza huduma karibu na wananchi.
Bi. Judica amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujali afya za Watanzania na watu wa Njombe kwa kuwaleta wataalam hao huku akiipongeza Wizara ya afya kwa kuja na ubunifu huo kwani watu wengi wa ngazi ya msingi wanahitaji huduma hizo kwa wingi.
Amesema Mkoa huo upo tayari kuanza zoezi hilo na wananchi wamekuwa wakiwasubiri kwa hamu kutokana na Wakurugenzi kuhamasisha zoezi hilo.
Bi. Judica amesema katika zoezi hilo mwaka uliopita walipata manufaa makubwa na wanashukuru kwa kuwa endelevu kwani limewasaidia wananchi kupata tiba za magonjwa mbalimbali na kupunguza rufaa sizizo za lazima.
“Mnafanya jambo la baraka kubwa na Mungu awabariki sana, naomba niwatie moyo, kuna changamoto mbalimbali naamini mnaenda kuzitatua na kuleta faraja kwa wananchi wa mkoa huu,” amesema Bi. Judica.
Amewataka watumishi wa afya katika eneo hilo kutoa ushirikiano kwa wataalam hao ili kusaidiana kutatua changamoto mbalimbali ambazo watazikuta na kuhakikisha wananchi wanapata tiba sahihi kwa wakati.
“Ninawaombeni sana mjitoe sana katika kuwaelewesha namna ya kutumia vifaa tiba vya kisasa ili viweze kutoa matokeo, tunataka ubora, ninawaomba sana wananchi wa Njombe Serikali inatoa huduma bora msikimbilie sehemu za ajabu ajabu au mitaani madaktari wapo twende kupimwa kwa usahihi upate tiba sahihi tunahitaji nguvu kazi ya taifa letu,”ametoa wito Bi. Judica.
Kwa upande wake Mratibu wa zoezi hilo kwa Mkoa wa Njombe Paschalina Endrew amesema kuwa zoezi hilo linalenga kuwasogezea Huduma wananchi karibu na maeneo yao ili kutopata hadha ya kufuata huduma za kibingwa na bingwa bobezi nje ya wilaya na mkoa wao na kuokoa muda wa rufaa za zisizo za lazima.
Naye mmoja wa Madaktari bingwa wa magonjwa ya masikio,pua na koo kutokea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Iringa, Dkt .James Msigwa amesema watakuwepo katika Hospitali zote za wilaya za mkoa huo kwa lengo la kuwapatia wananchi matibabu ya kibingwa na bingwa bobezi
Aidha Dkt. Msingwa amefafanua kwa kueleza kuwa kukoroma ni ugonjwa na unatibika hivyo wenye changamoto hiyo wafike kwa wingi ili kutibiwa kwa wakati.