Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

RAIS SAMIA KUENDELEA KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA MIPAKANI

Posted on: December 14th, 2023



Na. WAF, Kilimanjaro

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, Samia Suluhu Hassan amegawa magari 16 na Pikipiki 20  yakiwemo magari matatu  ya kubebea wahisiwa wa magonjwa ya kuambukiza ili kutatua changamoto ya usafiri kwa watumishi na kuongeza kasi ya huduma maeneo ya mipakani na viwanja vya ndege nchini. 

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel katika hafla ya kukabidhi magari na pikipiki kwa ajili ya kuimarisha huduma za afya mipakani katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, Mkoani Kilimanjaro

Dkt. Mollel amesema Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan chini ya Wizara ya Afya imeendelea kutekeleza afua mbalimbali za kudhibiti magonjwa kuenea ndani ya nchi yetu na kuzuia yasiingie au kuenea nje ya mipaka ya nchi.

“Hatua hii ni muhimu ili kutimiza Dira ya Sekta ya Afya ya kuwa na jamii yenye afya inayochangia ipasavyo katika ukuaji wa uchumi binafsi na uchumi wa nchi kwa ujumla”. Amesisitiza Dkt. Mollel

Aidha, amebainisha kuwa uwekezaji wa Rais Samia nchini ni jitihada za ukuaji wa uchumi Kitaifa na Kimataifa zinachochea ongezeko la safari za abiria na mizigo kutoka eneo moja hadi eneo jingine.

 Kwa wastani jumla abiria 114,000 kwa mwezi huwasili nchini kutoka nchi mbalimbali na pia wastani wa abiria 86,800 kwa mwezi husafiri nje ya nchi hasa kupitia uwanja wa ndege JNIA, Kiwanja cha ndege Kilimanjaro (KIA) pamoja na mipaka ya Namanga, Tunduma, Rusumo, Kasumulu na Mutukula.

Kwa kuzingatia umuhimu huo Wizara ya Afya inaendesha huduma za afya katika mipaka 54 inayojumuisha Viwanja vya ndege 13, Bandari 12 na Mipaka ya nchi kavu 29.

Huduma zinazotolewa katika ofisi za afya katika mipaka ni pamoja na Chanjo ya homa ya manjano, upimaji wa afya za abiria, ukaguzi wa vyombo vya usafiri pamoja na ukaguzi wa bidhaa mbalimbali ili kudhibiti kuenea kwa magonjwa.