Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

RAIS SAMIA AWATAKA WAFANYAKAZI HOSPITALINI KUFANYA KAZI KWA JUHUDI KUOKOA MAISHA YA WATU

Posted on: August 10th, 2022

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka wafanyakazi waliopo Hospitalini kufanya kazi kwa juhudi na kuokoa Maisha ya watu ili kuwa na jamii yenye afya bora.

Rais Samia amesema hayo leo mara baada ya kutembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe na kukagua ujenzi wa miundombinu iliyojengwa Hospitalini hapo kwa thamani ya Shilingi Bilioni 27.

“Wafanyakazi wa Hospitali nawashukuru sana, Mungu awatie nguvu muwahudumie wananchi, Mungu amekupanga hapo ili turudishe afya za Watanzania waweze kuingia mashambani, ofisini, waingie maeneo ya kazi tujenge taifa letu” amesema Rais Samia

Aidha Rais Samia amesema amesikia changamoto wanazokutana nazo watoa huduma za afya ikiwemo mahitaji ya vitendea na kuwaasa kuchapa kazi huku Serikali ikiendelea kushughulia changamoto hizo.

“Chapeni kazi, matakwa yenu tunayafahamu ikiwemo mahitaji ya vitendea kazi, tutakwenda kujitahidi kuyatimiza ili muweze kufanya kazi vizuri” Amesema Rais Samia

Kuhusu ujenzi wa miundombinu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe, Rais Samia amesema Serikali inatekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi inayoielekeza Serikali kusogeza huduma za afya karibu kwa wananchi.

“Tulitaka kufanya haya muda mrefu nyuma, kazi za Serikali ni hatua kwa hatua, kipindi hiki tumeweza kufanya haya na tunafanya kwa nchi nzima” amesema Rais Samia akiongelea miradi ya maendeleo katika Sekta ya Afya nchini.

Awali akizungumza, Waziri wa Afya Mhe Ummy Mwalimu amemshukuru Rais Samia kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya katika kuboresha Sekta ya Afya nchini.

“Kuna kazi kubwa inafanyika Mkoa wa Njombe ikiwemo kujenga Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya na hapa Hospitali ya Mkoa ambapo tumekamilisha ujenzi wa majengo” amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy amesema ujenzi wa hospitali hiyo ulianza Mwaka 2016 na hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 98 huku ukigharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 27.