PROF. JANABI ANATOSHA UKURUGENZI (WHO) AFRIKA- WAZIRI MHAGAMA
Posted on: March 22nd, 2025
Na WAF - DODOMA
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema Prof. Mohamed Janabi ni mtu sahihi ambaye anaweza kuongoza Sekta ya Afya Kanda ya Afrika kutokana na uzoefu wake.
Mhe. Mhagama amesema hayo Machi 22, 2025 Jijini Dodoma, katika mkutano wa waandishi wa habari ambao umelenga kutoa tamko rasmi la kumtambulisha Prof. Janabi na kuanza kwa kampeni ya kumnadi mgombea wa Tanzania ambaye atachuana na wagombea wengine watatu.
“Zipo sababu nyingi za Prof. Janabi kuwa Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika, miongoni mwa hizo ni Diplomasia ya nchi yetu kimataifa ambayo Rais wetu wa awamu ya Sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameitengeneza kimataifa na kuwezesha mataifa mengine kutambua weledi wetu kwenye sekta ya Afya” amesema Mhe. Mhagama.
Aidha, Waziri Mhagama amesema Prof. Janabi aliongoza mageuzi makubwa katika huduma za matibabu ya moyo nchini Tanzania na barani Afrika na hivyo kuwezesha kupunguza rufaa za nje ya nchi kwa asilimia 95 hali inayotoa taswira kuwa anaweza.
Mhe. Mhagama ameongeza kuwa, Prof. Janabi amefanya kazi kwa ukaribu na Mashirika ya Kikanda, Kimataifa, Serikali mbalimbali Barani Afrika na Ulimwenguni kote pamoja na Wadau wa Sekta ya Afya ili kuboresha upatikanaji wa huduma bora na endelevu za afya.
“Uzoefu wake wa kitaaluma na kiutendaji unampa sifa zinazohitajika kuongoza Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika kwa ufanisi mkubwa,” amefafanua Waziri Mhagama.
Mhagama amesema ni wakati sahihi wa nchi kusimama na Mgombea wake ambaye mbali na kuhudumu kwenye Sekta tofauti pia Prof. Janabi amekuwa mshauri wa karibu wa Viongozi wa juu akiwemo Rais Jakaya Kikwete na sasa Samia Suluhu Hassan.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika imempendekeza Prof. Mohamed Yakub Janabi, ambaye ni Mshauri wa Rais kwenye masuala ya afya na lishe kuwania nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika.