Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

PAC YAKOSHWA NA SERIKALI KUWEZESHA UZAZI SALAMA 16,851 HOSPITALI YA SEKOE TOURE

Posted on: March 26th, 2024



Na WAF - Mwanza

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali Mhe. Japhet Hasunga ameipongeza Serikali kwa kuboresha miundombinu ya afya hivyo kuwasaidia kinamama 16,851 kujifungua katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mwanza Sekou Toure tangu jengo jipya la mama na mtoto lilipozinduliwa.

Mhe. Hasunga amesema hayo leo Machi 26, 2024 alipowasili na wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali na kupokelewa na Katibu Mkuu Wizara ya afya Dkt. John Jingu kutembelea Mradi wa jengo la mama na mtoto lililogharimu zaidi ya billion 13.

Aidha, Mhe. Hasunga amesema kuwa Kamati yake imeridhishwa na mradi wa ujenzi wa jengo hilo ambalo Serikali imegharamia ujenzi huo kwa asilimia 100 hivyo ametoa rai kutunzwa kwa miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuipunguzia Serikali gharama za maboresho ya mara kwa mara.

“Kikubwa na kamati yangu tunapima thamani ya pesa kuona kama malengo yaliyokusudiwa yamefikiwa, na kwenye Hospitali yetu tumeona malengo yaliyokusudiwa yamefikiwa, kwa hiyo tunawapongeza ninyi kama Serikali kwa mradi na tuwaombe kuboresha miundombinu ili wakinamama waweze kuendelea kujifungua wakiwa salama”. Amesema Mhe. Hasunga

Kwa upande wake Katibu Mkuu wizara ya Afya Dkt. John Jingu amesema kuwa jengo hilo limeboresha huduma za Afya kwa kupunguzua msongamano na kuwezesha kutoa huduma za uzazi Staha ikiwa ni pamoja na kuhusisha faraja ya mwenza kwa wanaoridhia.

Pia, Dkt. Jingu amesema kuwa Mradi huo umeleta fursa za mafunzo kwa njia ya vitendo kwa watarajali takriban 200 kwa mwaka na wanafunzi wa vyuo mbalimbali ikiwa ni Pamoja na kuimarisha viwanda vya ndani kwa kufanya manunuzi mbalimbali.

Mwisho, Dkt. Jingu ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza ahadi kwa wananchi wa mkoa wa Mwanza ikiwemo ujenzi wa jengo la Mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou Toure- Mwanza ambapo baada ya kukamilika kwake huduma zimeanza kutolewa kwa wananchi.