Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

OMBWE LA WATUMISHI WA AFYA KUENDELEA KUTAFUTIWA UFUMBUZI

Posted on: August 14th, 2024

 


Na WAF – Dodoma


Serikali kupitia Wizara ya Afya imejipanga kutatua changamoto ya upungufu wa rasilimali watu na wahudumu wa Afya hususani kwenye maeneo ya vijijini ili kupunguza uhaba wa watumishi hao katika maeneo ya nje ya miji.


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Agosti 14,2024 wakati wakuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Baraza la Madaktari Tanganyika na baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania katika kumbi za Bunge Jijini Dodoma.

 

Waziri Ummy amesema hali ilivyo sasa, ambapo baadhi ya zahanati zina mhudumu mmoja pekee, ambaye analazimika kuhudumia wagonjwa wa nje, watoto, na pia akahudumie akina mama wanaojifungua. 


“Utakuta zahanati ina muuguzi mmoja, anawahudumie wagonjwa wa nje, aangalie watoto na kuwapa matone pia akawahudumia wakina mama wanaojifungua, mtaona kuwa huyu mhudumu anaelemewa na idadi kubwa ya watu." Amesema waziri Ummy


Aidha Mhe. Ummy ameishukuru Kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI kwa kupokea wasilisho ya baraza la Madaktari na Baraza la uuguzi na Ukunga Tanzania kwa mara ya kwanza kwakuwa kipindi cha nyuma haikuwahi kufanyika pamoja na kuona Afya ni jambo muhimu.


“Nipende kulipongeza bunge kwa kukubali na kukaa kusikiliza mawasilisho ya Mabaraza, kwani ni kwa mara ya kwanza kamati hii imepokea mawasilisho ya mabaraza na kujionea picha halisi kuhusu utaalamu na uhitaji wa wataalamu wenye vigezo vinavyohitajika kwaajili ya kutoa huduma bora za afya.” Amesema waziri Ummy