OCEAN ROAD INAPOELEKEA KUTIMIZA MIAKA 30 YAKUTANA NA WADAU
Posted on: August 29th, 2025
Na WAF, Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt. Diwani Msemo, leo Agosti 29, 2025 amekutana na wadau mbalimbali na kuzungumza nao juu ya namna wanavyoweza kushirikiana na Taasisi hiyo kuadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Msemo amesema kuwa maadhimisho hayo yatakayoshirikisha watu mbalimbali kutoka nchi zaidi ya 20 barani Afrika, hayatakiwi kuchukuliwa kama ni ya Taasisi ya Saratani Ocean Road peke yake bali ni ya wadau kwa ujumla wake.
Dkt. Msemo amesisitiza kuwa Taasisi ina hadithi nzuri za kusimulia kutokana na mafanikio makubwa iliyoyapata kutoka kutumia mashine za kizamani na sasa za kisasa kutokana na Serikali ya awamu ya sita ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambayo imewezesha kupatikana kwa mashine kadhaa ambazo zimekuwa mkombozi mkubwa wa changamoto ya Saratani kwa wananchi wa Tanzania.
Aidha Dkt Msemo amesema kuwa kwa nchi za Afrika ukitoa Afrika kusini, nchi inayoongoza kutoa huduma bora na zenye weledi za Saratani ni Tanzania.
Dkt. Msemo amewaomba wadau kutoa kama wanavyotoa nyakati nyingine, hivyo washirikiane ili kuwa na maadhimisho ya kipekee kabisa katika historia, tangu Taasisi hii ianzishwe.
Naye muwakilishi kutoka wizara ya Afya ambaye pia ni Mratibu wa Tiba Utalii nchini, Dkt. Asha Mahita ameipongeza Taasisi ya Saratani Ocean Road na kusisitiza kuwa wizara ya Afya ipo tayari kutoa msaada wa aina yoyote utakaohitajika kwani Wizara hiyo kama Mama wa ORCI imeona namna gani Taasisi inavyokimbia kwa kasi katika kuleta mapinduzi ya kweli kwenye matibabu ya Saratani.
Baadhi ya Taasisi zilizohudhuria ni BEACON, KAS MEDICS, eLIFE-LINE, SANLAM Insurance, BABUU CANCER FOUNDATION, Bodi ya Utalii Tanzania, Wizara ya Afya, Wizara ya Mambo ya Nje pamoja na Benki za NMB na NBC.