Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

NITASHUGHULIKIA HARAKA UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA

Posted on: January 11th, 2022

Na WAF - DODOMA 

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema atakwenda kushughulikia changamoto za utoaji wa huduma za Afya ambayo imekuwa ikilalamikiwa sana mitandaoni na kuripotiwa katika vyombo vya habari.

Waziri Ummy ameyasema hayo alipokutana na watumishi wa Wizara ya Afya mara baada ya kuapishwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma. 

"Katika ziara yangu ya kwanza nitaenda MSD kwa kuwa kuna malalamiko ya utoaji wa Dawa nikajue kuna tatizo gani." Amesema Mhe. Ummy.

Aidha, ameongeza kuwa pamoja na kuwepo UVIKO-19, lakini pia Magonjwa mengine kama malaria, kifua kikuu, kipindupindu na na mambo yote yanayohusu Afya inabidi yaendelee kuchukuliwa kwa uzito sawa kwani ni magonjwa ambayo yanaendelea kuisumbua jamii.

Hata hivyo       Waziri Ummy amesema katika kuelekea katika mfumo wa Bima ya Afya kwa wote atakwenda kushughulikia haraka jambo hilo ili kuwawezesha wananchi wa hali ya chini kupata huduma kwa wepesi.

Kwa upande wake Naibu waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ametoa pongezi kwa wote walioteuliza na kuaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kufanya nae kazi.

"Mhe. Waziri pia nikupongeze kwa kurejea na nashukuru umenikuta kwakuwa tulishafanya kazi pamoja nikuahidi tutaendelea kuwa pamoja na niko tayari kutumwa nitatumika." amesema Dkt. Mollel.

Nae katibu mkuu wizara ya Afya Prof. Abel Makubi ametoa pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwateua na kuwaamini viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Afya mhe. Ummy Mwalim.

"Lakini nikupongeze Mhe. Waziri kwa kupata teuzi hii pia nikuahidi niko tayari kutumika na nitatoa ushurikiano ili kufikia malengo ya Wizara." amesema Prof. Makubi

Hafla hiyo fupi ya kumpongeza na kumkaribisha Waziri Ummy  ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel, Katibu Mkuu Prof. Abel Makubi, wakurugenzi na watumishi kutoka wizara ya Afya.

MWISHO