Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI ZAJADILIANA KUANZISHA VITUO VIWILI VYA UMAHIRI TANZANIA

Posted on: June 14th, 2024


Na WAF - Arusha


Wataalam wa Sekta ya Afya kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wajadiliana kuanzishwa kwa kituo cha umahiri cha Sayansi ya Afya ya Kinywa chini ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) pamoja na kituo cha umahiri cha upandikizaji Uloto na matibabu ya Magonjwa ya Damu kinachosimamiwa na Hospitali ya Benjamin Mkapa nchini Tanzania.


Majadiliano hayo yanaendelea leo Juni 14, 2024 Jijini Arusha ikiwa ni siku ya Pili ya kikao hicho ambacho kimewakutanisha Makatibu Wakuu kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa lengo la kujadiliana namna ya kukabiliana na changamoto kubwa za kiafya.


Wakati wa kikao hicho Naibu Katibu Mkuu Dkt. Grace Magembe aliyeambatana na Prof. James Mdoe Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema vituo hivyo vitasaidia kuboresha kwa kiasi kikubwa uwezo wa kutoa matibabu ya Kibingwa, mafunzo ya ubobezi pamoja na utafiti katika nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).


“Wakati tunaendelea na ajenda ya leo, naomba tujadili kwa kina kuhusu dhana ya kuanzisha Kituo cha umahiri cha Sayansi ya Afya ya Kinywa kitasimamiwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) pamoja na kituo cha umahiri cha upandikizaji Uloto na Sayansi ya matibabu ya magonjwa ya damu kitasimamiwa na Hospitali ya Benjamin Mkapa.” Amesema Dkt. Magembe


Aidha, Dkt. Magembe amesema kuanzishwa kwa vituo hivyo ni kuonesha ushirikiano wa Kikanda katika Jumuiya ambapo wataalam kutoka katika vituo hivyo watatumika kama vitovu vya uvumbuzi pamoja na kufanya kazi kwa ushirikiano na vituo vingine vya ubora vya Kikanda (RCoE) wakitumia maarifa na rasilimali za pamoja ili kukabiliana na changamoto za Afya.


Mwisho Dkt. Magembe amezitaka Nchi wanachama na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kushirikiana katika kuharakisha utekelezaji wa maagizo ya mkutano huu ili kufikia malengo yaliyowekwa kwa manufaa ya wananchi wa Jumuia.