Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MUHIMBILI YASHIKA NAFASI YA PILI USHINDI WA JUMLA BANDA BORA SABASABA 2024

Posted on: July 3rd, 2024Hospitali ya Taifa Muhimbili leo imefanikiwa kupata tuzo ya nafasi ya pili, mshindi wa jumla kwenye banda bora katika maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam kwa mwaka 2024 ambayo imepokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo Prof. Mohamed Janabi.


Tuzo hiyo imetolewa na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Mhandisi Filipe Jacinto Nyusi ambaye alikua mgeni rasmi katika ufunguzi wa maonesho hayo akiwa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Tuzo hiyo imetokana na namna watoa huduma wa hospitali hiyo wanavyotoa elimu, ushauri na huduma bora za ubingwa bobezi kwenye banda namba 16 la hospitali hiyo linalopatikana Mtaa wa Biashara katika maonesho hayo. 


“Kwakweli tumefurahi sana, ahadi yetu kwa Uongozi na Watanzania ni kuendelea kutoa huduma bora na tunaamini mwakani tutafanya vizuri zaidi na kuendelea kuwadhihirishia watanzania sisi ni vinara na mwongoza njia katika huduma za afya nchini,” wamesisitiza watoa huduma wa hospitali katika banda hilo.