Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MUHIMBILI YAPELEKA MSAIKOLOJIA TIBA KATESH NA MSAADA WA DAWA ZA TZS. 38 MIL

Posted on: December 8th, 2023


Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeungana na wananchi wa Mji mdogo wa Katesh Wilayani Hanang, Mkoani Manyara na kupeleka msaada wa dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya TZS. 38 Mil ili kusaidia jitihada za utoaji huduma katika eneo hilo, ambalo hivi karibuni lilikumbwa na maafa ya mafuriko yaliyosababisha maporomoko ya udongo kutoka mlima Katesh na kuleta madhara makubwa ikiwemo vifo, majeruhi, upotevu wa mali na uharibifu wa miundombinu.


Akizungumza kwa Niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Mkuu wa Idara ya Famasi, Mfamasia. Nelson Faustine amesema sambamba na msaada huo, Hospitali imetuma Msaikolojia Tiba kwenda kuungana na timu za watalam mbalimbali walioko kule wanaotoa huduma kwa waathirika wa mafuriko hayo.


Hatua hii pia ni kuitikia wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameagiza kupelekea watalaam wa saikolojia kuzungumza na wananchi waliopata mfadhaiko kutokana na tukio hilo ili waweze kurejea katika hali ya kawaida.


Bodi ya Wadhamini, Menejimenti na Wafanyakazi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wanaendelea kutoa pole kwa wananchi wa Mji mdogo wa Katesh Wilayani Hanang, Mkoani Manyara kutokana na madhara waliyopata.