Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADAKTARI BINGWA 56 WAKITA KAMBI MOROGORO, KUHUDUMIA KANDA YA KATI, KUWAFIKIA WANANCHI ZAIDI YA 2000.

Posted on: April 29th, 2024Na WAF - Morogoro

Madaktari bingwa 56 wanatarajiwa kushiriki kutoa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi kwa wananchi zaidi ya 2000 kutoka Mikoa ya Morogoro, Iringa, Singida, Dodoma na Pwani kupitia kambi ya maalum ya matibabu ya siku tano na madaktari bingwa wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ndani ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.

Hayo ameyasema Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima leo tarehe 29 Aprili, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa Habari mkoani hapo.

Amesema Kambi hiyo maalum inayotarajiwa kuanza tarehe 6 Hadi 10 Mei, 2024 inamsaada mkubwa kwa wananchi na kuongeza kuwa zaidi ya huduma ya upasuaji 100 zitatolewa kwa wagonjwa.

“Wananchi watapata huduma za kibingwa kwa uharaka zaidi na kwa ukaribu kupitia kambi hii maalum ya Madaktari bingwa wa Rais Dkt. Samia. Pia nichukue fursa hii Kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan misingi ya kuthamini watanzania na niwashukuru madaktari hawa kwa kujitoa kwao kuiheshimisha serikali na kuwapa afua wananchi”. Amesema Mhe Malima

Aidha amevitaka vyombo vya habari kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kuja kupima afya zao ndani ya kambi hiyo maalum na kulipa kipaumbele jambo hilo ili kuhakikisha inawafikia watu wengi zaidi.

Ameongeza kwa kutoa ombi kwa wakuu wa mikoa hiyo mitano tano na wakuu wa wilaya pamoja na wabunge kushirikiana kwa pamoja kutoa hamasa kwa wananchi.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro Dkt. Daniel Nkungu amesema Hospitali hiyo kama mwenyeji wa Kambi maalum imejipanga kikamilifu na kuongeza kuwa katika kuhakikisha kila mwananchi aliyejiandikisha anapata huduma hiyo kutakuwa na ongezeko la muda endapo kutakuwa na wagonjwa wamebaki na hawakupatiwa huduma baada ya muda wa siku tano kuisha.

Dkt. Nkungu ametoa rai kwa wanawake kujitokeza kwa wingi ili waweze kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya wanawake na mingine.