Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MOI YAPOKEA MADKTARI BINGWA WA MIFUPA KUTOKA CHINA

Posted on: January 29th, 2024

Taasisi ya tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imepokea madaktari bingwa wa mifupa na ubongo kutoka Jamhuri ya Watu wa China wakaohudumu kwa kipindi cha miaka miwili ikiwa ni muendelezo wa ushirikiano baina ya Tanzania na China.

Akizungumza leo Januari 29, 024 wakati wa hafla fupi yakuwapokea madaktari hao kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Mkurugenzi wa Upasuaji wa Ubongo wa MOI Dkt. Lemeri Mchome ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Watu wa China na kuongeza kuwa ujio huo utaongeza ujuzi na umahiri kwa madaktari wazawa.

“Wenzetu China wamepiga hatua katika tiba za mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu, hivyo uwepo wao hapa utasaidia kuwajengea uwezo kwa madaktari wetu, ninaaamini walivyotukuta sivyo ndivyo watakavyotuacha, umahiri wetu utakuwa umepanda” amesema Mchome

Kwa upande wake mwenyeji wa madaktari hao Dkt. Liggy Vumilia kutoka wizara ya afya amesema madaktari hao 11 watakuwapo nchini kwa miaka miwili wakitoa huduma katika Taasisi ya MOI, hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya.

“Tanzania na China zimekuwa katika uhusiano kwa zaidi ya miaka 60 sasa…ujio wa madaktari hawa ni muendelezo wa ushirikiano huo, wito wangu kwenu kuhakikisha mnawatumia vyema madaktari hawa ili tupate ujuzi walio nao, ni imani ya wizara kuwa huduma zetu zitaboreshwa kwa kuwatumia vizuri madaktari hawa”

Mratibu wa Mafunzo na Utafiti wa MOI Dkt. Joel Bwemelo amesema ujio wa madaktari bingwa hao unalenga kubadilishana uzoefu wa kutoa tiba kwa ufaninsi na hivyo kuboresha huduma kwa wagonjwa.

“Tumepokea madaktari bingwa watatu, mmoja wa usingizi, mwingine wa mifupa na wa tatu ni wa ubongo, wawili watakuwapo hapa kwa mwezi mmoja na nusu kabla ya kwenda hospitali ya rufaa Mbeya, na huyu mmoja atakuwa MOI kwa miaka yote miwili.

Kiongozi wa madaktari hao Dkt. Cheny Jiyong ameishukuru MOI kwa mapokezi na kuahidi kutoa ushirkiano wa dhati katika kutekeleza majukumu yao.