Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MKUU WA USHIRIKIANO WA MAENDELEOWA UBALOZI WA CANADA AAGANA NA KATIBU MKUU DKT. JINGU

Posted on: June 25th, 2024

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu leo Juni 25, 2024 amekutana na kufanya mazungumzo na Bi. Helen Fytche ambaye ni Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Ubalozi wa Canada kwa ajili ya kumuaga baada ya kufanya kazi nchini kwa miaka mitatu.

Dkt. Jingu amemshukuru Bi. Helen kwa niaba ya Serikali ya Kanada na jitihada zake binafsi katika kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha huduma za afya nchini.

Dkt. Jingu amemweleza juu ya jitihada zinazoendelea katika kuhakikisha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa wote unaanza mara moja na kuiomba Serikali ya Kanada kuendelea kusaidia mikakati inayoendelea ya kuongeza idadi ya wahudumu wa afya kuanzia ngazi ya jamii ili kufikia malengo yaliyowekwa.

Aidha, Katibu Mkuu huyo ameiomba Serikali ya Kanada kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kubadilishana Watalaam kwa ajili ya kuongeza ujuzi na ubobevu wa kutoa huduma za afya nchini.

Kwa upande wake Bi. Helen ameipongeza Wizara ya Afya kupitia kwa Katibu Mkuu Dkt. John Jingu kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya Afya chini ya uongozi wake na kujifunza juu ya kujitoa kwa viongozi wa Wizara ya Afya na watumishi wa sekta ya afya katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za Afya.

“Nimeshuhudia mafanikio makubwa katika sekta ya Afya hapa Tanzania, huduma za afya katika ngazi ya msingi zimendelea kuimarika kutokana na usimamizi mzuri wa fedha za Mfuko wa Afya wa Pamoja ambazo Kanada ni mojawapo ya nchi zinazotoa fedha kwa ajili ya Mfuko huo, uwanzishwaji wa mpango Jumuishi wa Kitaifa wa wahudumu wa Afya ngazi ya jamii ambao utasaidia kuongeza mapambano ya kukabiliana na magonjwa ya milipuko na magonjwa mengine pamoja na kupitishwa kwa sheria ya Bima ya Afya kwa wote na mikakati iliyofanyika ya kuanza utekelezaji wake”. Amesema Bi. Helen.

Mwisho ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya juu ya juhudi mbalimbali zinazoendelea katika kuboresha mifumo ya utoaji wa huduma za afya nchini.