MIUNDOMBINU SEKTA YA AFYA PERAMIHO YAZIDI KUIMARIKA
Posted on: September 24th, 2024Na WAF - Peramiho, Ruvuma
Serikali kupitia Wizara ya Afya imetoa shilingi Bilioni 40 kwa mwaka wa fedha 2023/24 ili kuendelea kuimarisha miundombinu ya miradi mbalimbali ikiwemo ya Sekta ya Afya kwa kujenga Hospitali pamoja na vituo vya Afya katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma ikiwa pamoja na Jimbo la Peramiho.
Waziri wa Afya na mbunge wa jimbo la Peramiho Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Septemba 24, 2024 wakati wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Jimbo la Peramiho, Songea Mkoani Ruvuma.
"Kwa Mwaka wa fedha 2023/24 Serikali imetoa fedha kiasi cha Tsh: Bilioni 40 katika Jimbo la Peramiho ili kutekeleza miradi ya maendeleo katika Sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Afya kwa kujenga Hospitali pamoja na Vituo vya Afya." Amesema Waziri Mhagama
Aidha, Waziri Mhagama amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kufanya kazi na Hospitali ya St. Joseph's Mission ya Peramiho kama Hospitali ya Rufaa ya ngazi ya mkoa ambapo hadi sasa Serikali imetoa shilingi Bilioni 3.2 ili kuisaidia Hospitali hiyo.
"Mhe. Rais kwakweli nakushukuru sana kwa kuendelea kuniamini kuwa katika Serikali yako, nakuahidi nitafanya kazi usiku na mchana ili kukusaidia katika Sekta ya Afya, sitakuangusha naomba Mungu anisaidie." Amesema Waziri Mhagama
Waziri Mhagama amesema, maelekezo aliyoyatoa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni lazima yatekelezwe ikiwemo ukamilishaji wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma ili wananchi wasipate adha ya kufuata huduma za Afya mbali na makazi yao.
"Mhe. Rais nikupongeze na nikushukuru kwa kuendelea kuimarisha miundombinu ya Sekta ya Afya nchini ikiwemo kuongeza madaktari wa ubingwa bobezi, vifaa pamoja na vifaa tiba." Ameeema Waziri Mhagama
Mwisho, Waziri mhagama amesema, kutokana na gharama za matibabu kuwa kubwa, Serikali kupitia Wizara ya Afya imeamua kuja na Bima ya Afya kwa wote ili wananchi wapate huduma hadi kufikia Hospitali ya Taifa Muhimbili bila kuwa na kikwazo cha fedha.