MIKAKATI INAHITAJIKA KUPUNGUZA VIFO VYA UZAZI, WATOTO WACHANGA.
Posted on: April 3rd, 2025
Na WAF, Singida
Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Fatma Mganga amewataka viongozi wa sekta za afya ngazi za mikoa kuutumia mkutano wa mwaka wa kutathimini huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto kanda ya kati kutafakari na kupanga mikakati kabambe inayotekelezeka ya kuboresha huduma ili kuendelea kupunguza vifo vinavyotokana na na uzazi, mama na mtoto.
Dkt. Mganga ameyasema hayo Aprili 3, 2025 mkoani Singinda katika mkutano wa mwaka wa kutathimini huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto kwa mikoa ya kanda ya kati inayobeba mkoa wa Singida, Manyara na Dodoma unaoenda sambamba na kauli mbiu “Uongozi na uwajibikaji ni chachu katika kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi na vifo vya watoto”
Dkt. Mganga amesema mkutano huo uhakikishe unatoka na maazimio na mikakati tofauti yenye ubunifu ndani yake ili kuleta matokeo mazuri na kuwezesha watu wengine kwenda kujifunza kanda ya kati.
Amesisitiza ni jukumu la viongozi kusimamia uwajibikikaji wa watumishi kwa kuzingatia miongozo, kanuni na sheria ili kutimiza majukumu yao, kupunguza kabisa vifo vya mama na mtoto na kuendana na thamani ya uwekezaji wa vifaa tiba vya kisasa pamoja na miundombinu na watumishi uliofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya Afya nchini.
Aidha, Dkt. Mganga ameeleza kuwa Kanda ya Kati ina jumla ya vituo vya kutolea huduma za Afya vipatavyo 1527, ambapo vituo vinavyotoa huduma ya upasuaji wa dharura kwa akina mama wajawazito vimeongezeka kutoka vituo 44 kwa mwaka 2021 hadi vituo kufikia 107 kwa mwaka 2023, lengo likiwa ni kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi na vifo vya watoto wachanga.
Akitoa salamu za Wizara za Afya kutoka Idara ya Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto Dkt. Ismail Mtitu amesema Wizara ya afya inatambua mchango wa viongozi na watumishi wa sekta ya afya katika kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi, mama na mtoto na kuongeza kuwa lengo kubwa mkutano huo ni kujadili utekelezaji wa afua mbalimbali zinazotekelezwa na Wizara ya Afya zinazolenga kuboresha huduma za mama na mtoto.