MIAKA 30 YA MOI KWENYE UMAHIRI, YAKUSANYA RASILIMALI KUSAIDIA WATOTO WENYE CHANGAMOTO ZA AFYA
Posted on: October 25th, 2026Na Hassan Kimweri, WAF - Dar es Salaam
Maadhimisho ya miaka 30 ya umahiri katika huduma za kibobezi za mifupa na mfumo wa fahamu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) ni fursa muhimu ya kutambua mchango wa taasisi hiyo katika kutoa huduma za kibingwa kwa Watanzania na wananchi kutoka nje ya mipaka ya nchi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe, amesema hayo leo Oktoba 25, 2026 wakati wa mbio za kuadhimisha miaka 30 ya MOI, huku akiwapongeza washiriki wote walioshiriki katika mbio hizo kwa lengo la kuchangisha fedha zitakazosaidia matibabu kwa watoto wenye changamoto za kiafya.
"Fedha zitakazopatikana kupitia mbio hizo zitaelekezwa kusaidia matibabu ya ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu, hususan kwa watoto wenye changamoto za kiafya ikiwemo vichwa vikubwa na mgongo wazi ili kuwapa nafasi ya kupata matibabu na kuishi maisha yenye matumaini kama watoto wengine," amesemq Dkt. Magembe
Aidha, Dkt. Magembe ametumia jukwaa hilo kusisitiza umuhimu wa wananchi kujiunga na bima ya afya kwa wote ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu bila ya kikwazo cha fedha kipindi cha kuugua, kuepuka ulaji wa vyakula vyenye sukari nyingi, chumvi na mafuta ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza pamoja na kuacha tabia ya kuwaficha watoto wenye changamoto za kiafya.
Dkt. Magembe amewashukuru wadau mbalimbali, wakiwemo benki, taasisi na wananchi walioshiriki katika kufanikisha maadhimisho hayo, akibainisha kuwa ushirikiano kati ya Serikali na wadau ni muhimu katika kuboresha huduma za afya na kupunguza changamoto zinazowakabili watoto wanaohitaji matibabu ya kibingwa.
"Tunaomba wadau wengine waendelee kujitokeza kufadhiri kwa kuwa gharama za matibabu kwa baadhi ya watoto wenye changamoto hizo ni kubwa, hivyo ushiriki wa wadau katika kuchangisha fedha ni hatua muhimu ya kusaidia familia zinazokabiliwa na changamoto za kifedha na kuhakikisha watoto wanapata huduma wanazohitaji," amesema Dkt. Magembe