Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MHE. UMMY AHIMIZA WATUMISHI AFYA CALL CENTRE 199 KUONGEZA UFANISI KUHUDUMIA WANANCHI

Posted on: July 4th, 2024

.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (Mb) amefanya ziara ya kikazi katika Kituo cha Kupokea na Kujibu hoja za Wananchi cha Wizara ya Afya (Afya Call Centre 199) kwa lengo la kufuatilia utendaji na ufanisi wa huduma zitolewazo kwa wananchi.

Akiwa katika ziara hiyo leo Julai 4, 2024 katika kituo hicho Mhe. Ummy Mwalimu amewapongeza watumishi wanaofanya kazi katika kituo hicho, akiwataka kuongeza juhudi na ufanisi katika kuhudumia wananchi na pia kuzingatia huduma bora kwa mteja, kutoa taarifa kwa usahihi na kwa wakati na kutumia muda kuwaelimisha wananchi wanaopiga simu kituoni hapo. 


Aidha, Mhe Waziri Ummy pamoja na kukagua kazi zinazofanyika, alipata wasaa wa kufanya kikao na watumishi hao kusikiliza changamoto zao na maboresho ambayo wangependa yafanyike, utaratibu ambao Mhe Ummy amekuwa akifanya kwa Idara na vitengo mbalimbali ndani ya Wizara.

"Naibu Katibu Mkuu Dr Grace uko hapa, umeona na kusikia kazi kubwa inayofanyika katika kituo hiki na ongezeko la mahitaji ya rasilimali ikiwemo fedha, watumishi na vifaa, maagizo yangu kaeni na kituo hiki na kuja na mapendekezo ya namna bora ya kuboresha upatikanaji wa fedha, watumishi na rasilimali nyingine ili kuongeza ufanisi wa kituo hiki", alisema Mhe. Ummy

Nae Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt.Grace Magembe alimuhakikishia Mhe Waziri kuwa maelekezo yake yatafanyiwa kazi kwa ukamilifu na tayari kuna baadhi ya maboresho yameanza kufanyika na kabla ya terehe 15/07/2024 kikao cha pamoja na watumishi hao kitafanyika. 


Kituo hicho kinatoa taarifa mbalimbali kwa wananchi kwa njia ya simu na jumbe kwa lengo la kuelimisha umma ili kuwaepusha wananchi na tabia hatarishi zinazochangia kuongezeka na kuenea kwa magonjwa mablimbali ya kuambukiza na yasiyo ambukiza na pia wanapokea changamoto na pongezi zinazoelekezwa kwenye sekta ya afya kutoka kwa wananchi.


Akitoa taarifa mratibu wa kituo hicho Bi Beatrice salanga alisema kwa siku wanapokea simu. wastani kati ya Simu 2,000 hadi 3,000 kutoka maeneo mbalimbali na kuahkikisha wanapata ufumbuzi wa kila jambo kupitia Idara na vitengo mbalimbali vilivyoko chini ya Wizara ya Afya.