Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MGANGA MKUU WA SERIKALI ATAKA MBINU MPYA KUKABILIANA NA MALARIA, UKIMWI NA KIFUA KIKUU

Posted on: March 22nd, 2024


Na WAF - DODOMA

Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Tumaini Nagu amewataka wajumbe wa Mkutano wa Mpango mkakati wa kutekeleza afua zilizodhaminiwa na fedha za Mfuko wa Dunia mzunguko wa saba kubadili mbinu na mikakati ili kukabiliana na magonjwa ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria.

Prof. Nagu ameyasema hayo Machi 22, 2024 wakati akifunga Mkutano wa wadau wa utekelezaji wa afua za fedha za Mfuko wa Dunia katika kukabiliana na Magonjwa hayo uliokua unafanyika jijini Dodoma.

“Tukitumia mbinu na mikakati ya zamani hatutaweza kufanikiwa lakini kama tutabadili na kuja na mikakati mipya tutafanikiwa tunapokwenda kuanza upya utekelezaji wa afua za mapambano dhidi ya magonjwa hayo”. Amesema Profesa Nagu.

Profesa Nagu amesema Mpango wa Dunia kujitathmini ni mwaka 2025 hadi 2030 lakini kama nchi lazima ijitathmini ifikapo 2026 kwa mantiki hii lazima mbinu na mikakati iwe inayoweza kupimika.

Prof. Nagu ameongeza kuwa Mawaziri wa nchi zinazokabiliwa na Malaria walishakubaliana kuwa na ziro Malaria katika nchi zao ikiwemo Tanzania hivyo ametoa rai kwa wale wanaoshughulika na afua ya Malaria waweke mikakati inayopimika.

Amezitaka Halmashauri kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI kuona umuhimu wa kutenga fedha kwa ajili kununua dawa za kukabiliana na vyanzo vya mazalia ya mbu wasababishao malaria ikiwepo kunyunyiza dawa huku akihimiza wananchi kuweka mazingira safi.

Kuhusu UKIMWI, Prof. Nagu amesema bado hali sio nzuri kwenye huduma za mama na mtoto kwani watoto hawajafatiliwa vya kutosha mara baada ya kuzaliwa na kuhakikisha wana hudhuria kliniki kwa wiki zote zinazo elekezwa kitaalam.

Kuhusu kifua Kikuu, ametaka kuimarishwa kwa vipimo ndani ya nchi ili isitokee kesi ya mtu kuanzishiwa matibabu ya kifua kikuu bila uthibitisho wa maabara.

“Nakumbuka ilitokea mgonjwa mmoja alikuwa amepimwa akaonekana na kifua kikuu lakini, alivyo fanyiwa vipimo zaidi ikabainika ni kansa, sasa vema tukajiridhisha ipasavyo kabla mgonjwa hatujaanza kumtibu”. Amesema Prof. Nagu.