Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MAZOEZI NI TIBA KILA MMOJA AONE WAJIIBU: WAZIRI UMMY

Posted on: May 16th, 2024


Na WAF - Dar Es Salaam


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ametoa wito kwa Watanzania kuzingatia mtindo bora wa maisha ikiwemo ulaji wa vyakula pamoja na kufanya mazoezi ili kuepuka madhara ya kukatwa viungo.


Waziri Ummy amesema hayo leo Juni 16, 2024 wakati aliposhiriki jogging iliyoongozwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ya Kilomita Tano kuanzia katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe hadi Tangi Bovu mbezi na kurejea viwanja vya Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam.


"Madhara ya kutofanya mazoezi ni makubwa sana, Watu wanapata magonjwa ya moyo, Kisukari pamoja na Shinikizo la Juu la Damu kutokana na tabia bwete na kutozingatia ulaji wa vyakula unaofaa." Amesema Waziri Ummy


Amesema, hata kama una Kisukari au ugonjwa wa Shinikizo la Juu la Damu, ukifanya mazoezi unazuia usiende katika hatari kubwa ikiwemo ya kukatwa viungo kama miguu au kufanyiwa upasuaji wa moyo ambao unagharama zaidi ya Milioni 30 au 40.


"Kinga ni bora kuliko tiba, tumeamua kama Wizara ya Afya kuwaunga mkono Efm kwa sababu tunatekeleza kampeni yetu ya Mtu ni Afya, Afya yako wajibu wako." Amesema Waziri Ummy


Ikiwa ni siku ya Wababa Duniani, Waziri Ummy amewakumbusha wakina baba wote kuwasindikiza wake zao kwenda cliniki ili kuwajibika katika malezi, makuzi na maendeleo ya watoto wao.