MAZINGIRA RAFIKI KWA WANAWAKE KUNYONYESHA MAENEO YA KAZI NI MUHIMU
Posted on: August 7th, 2024
Na WAF – Dodoma
Waajiri katika sekta rasmi na zisizo rasmi wamehimizwa kuwawekea mazingira rafiki wanawake wenye watoto ili waweze kunyonyesha watoto wao katika maeneo yao ya kazi.
Hayo yamesemwa leo, Agosti 6, 2024, na Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Afya, Bi. Grace Sheshua, wakati akifungua mkutano wa maafisa rasilimali watu na sheria kutoka taasisi na mashirika ya serikali kuhusu masuala ya unyonyeshaji maziwa kwa wamama mahali pa kazi.
“Lishe ya mtoto katika siku 1000, yaani tangu kutungwa kwa mimba hadi mtoto anapofikisha umri wa miaka miwili, ndiyo msingi bora wa ukuaji wa mtoto kimwili na kiakili, amesema na kuongeza
"Madhara ya lishe duni, hasa udumavu, yanaathiri sana maendeleo ya rasilimali watu ya nchi hivyo ni muhimu kwa mtoto kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo na kuendelea kunyonyeshwa huku akipatiwa chakula cha nyongeza hadi anapotimiza miaka miwili au zaidi,” amesisitiza Bi. Grace.
Aidha, Bi. Grace amesema unyonyeshaji maziwa ya mama ni njia bora na salama ya kulisha watoto na mojawapo ya uwekezaji muhimu wa gharama nafuu unaoweza kufanyika kwa taifa lolote kwa mustakabali wa jamii bora kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kanda ya Kati wa TAWLA, Bi. Neema Mushi, amesema changamoto nyingine ni ukiukwaji wa haki za uzazi za wanawake wanaofanya kazi katika baadhi ya sekta rasmi na sekta zisizo rasmi. Hii inatokana na kukosekana kwa mazingira wezeshi katika mifumo ya kijamii ya kuwasidia wanawake waweze kuwanyonyesha watoto wao ipasavyo.
Naye Bi. Grace Moshi, Afisa Lishe kutoka Wizara ya Afya, ameeleza umuhimu wa lishe bora kwa mama mjamzito na anayenyonyesha, akisisitiza kuwa maandalizi mapema ni muhimu ili kuepuka changamoto kama ukosefu wa maziwa ya kutosha. Alizungumzia pia kuhusu faida za maziwa ya mama kwa afya ya mtoto, na umuhimu wa mtoto kunyonya maziwa hayo kwa miezi sita bila kuongezewa vyakula vingine.