Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MATUMIZI SAHIHI YA KONDOMU YATATULINDA DHIDI YA MARADHI

Posted on: February 14th, 2025

Na WAF - Dodoma

Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Bi. Ziada Sellah amewahimiza watanzania wote kuzingatia matumizi sahihi na endelevu ya Kondomu na njia nyingine za kujikinga dhidi ya maambukizi ya VVU na magonjwa ngono ili kulinda afya.

Bi Ziada ametoa rai hiyo Leo Februari 13, 2025 alipo wakilisha Salaam za Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe wakati wa Maadhimisho ya siku ya Kondomu Duniani yanayofanyika Jijini Dodoma kitaifa.

"Nitoe rai kwa watanzania wenzangu tuzingatie njia za kujilinda dhidi ya maambukizi ya VVU na magonjwa ngono kwa kufanya matumizi sahihi ya Kondom, lakini pia kuwa na mwenza mmoja mwaminifu na unayejua hali yake ya kiafya lakini kwa wenye maambukizi wafanye matumizi ya dawa kinga ya PrEP," amesema Bi Ziada.

Aidha Bi ziada amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau imesambaza Kondomu za kiume 94,086,400 katika vituo vya kutolea huduma za afya, ngazi ya jamii na mahali pa kazi katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2024 ikiwa ni juhudi za kuendelea mapambano ya Virusi vya UKIMWI.

"Kwa mwaka 2024 Kondomu Kondomu 30,342,204 ziliuzwa kwa bei yabpunguzo na Kondomu zipatazo 7,126,164 zimeuzwa kwa bei ya kibiashara kuhakikisha kila mtu anapata kutokana na uwezo wake," amesema Bi. Ziada.

Kwa upande wake Kaimu Meneja mpango wa Taifa wa kudhibiti UKIMWI Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini Dkt. Zeye Nkomela amesema Serikali imejipanga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya ikiwemo upatikanaji wa huduma ya Kondomu bure na kwa gharama nafuu maeneo yote nchini.