MATOKEO YA UTAFITI KUBORESHA HUDUMA ZA WATOTO WACHANGA
Posted on: October 27th, 2026Na Hassan Kimweri, WAF – Dar es Salaam
Matokeo ya tafiti za afya ni muhimu katika kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi hususan watoto wachanga waliozaliwa kabla ya wakati na wenye uzito pungufu ambao wako katika hatari kubwa ya kupata maambukizi na changamoto nyingine za kiafya.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe, amesema hayo leo Oktoba 27, 2026 wakati akifungua kongamano la kuwasilisha na kusambaza matokeo ya tafiti za kitaaluma katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), jijini Dar es Salaam.
Kongamano hilo limehusisha usambazaji wa matokeo ya utafiti na uzinduzi wa kifurushi cha huduma za kusaidia ulishaji wa watoto wachanga katika vituo vya afya, kinachojulikana kama 'Facility-Based Feeding Support Package Plus (FSB Plus)' ili kuwasaidia watoto hao wanaozaliwa na uzito pungufu au kabla ya wakati kuwa katika hali ya kawaida.
"Utafiti uliofanyika Tanzania, Malawi na India umeongeza uelewa kuhusu unyonyeshaji, ukuaji na changamoto za kiafya kwa watoto waliozaliwa kabla ya wakati na wenye uzito upungufu, ni muhimu sana kuhakikisha kila mtoto anapata huduma stahiki tangu anapozaliwa ili kuongeza nafasi zake za kuishi na kukua vizuri," amesema Dkt. Magembe
Aidha, Dkt. Magembe amesisitiza kuwa watoa huduma za afya wanapaswa kuwasaidia akina mama wanapojifungua kuanza kuwanyonyesha watoto mapema iwezekanavyo na kutoa mwongozo sahihi kwa watoto ambao hawawezi kunyonya moja kwa moja.
Dkt. Magembe ameeleza kuwa Wizara ya Afya itapokea matokeo ya utafiti huo kwa ajili ya kupitia na kuboresha miongozo na taratibu za utoaji huduma, huku akiwahimiza watoa huduma za afya kubadili utendaji wao kwa kuzingatia ushahidi wa kisayansi na kutoa mrejesho kuhusu changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji.
"Wazazi na walezi wanapaswa kueleweshwa namna hatua zinazochukuliwa zinavyosaidia kulinda afya na maisha ya watoto wao, Serikali inaendelea kupanua huduma za watoto wachanga nchini ambapo idadi ya NCU zimeongezeka kutoka 14 mwaka 2018 hadi kufikia 432 mwaka 2026," amesema Dkt. Magembe