Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MASHINE 263 ZA KUNYUNYIZIA VIRUTUBISHI ZIMEFUNGWA MIKOA 26

Posted on: May 14th, 2024

UTEKELEZAJI WA BAJETI YA WIZARA YA AFYA 2023/24


Na WAF - Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya inahamasisha kufungwa mashine za kunyunyiza virutubishi (dosifiers) kwenye vyakula ambapo hadi sasa jumla ya mashine 263 zimefungwa katika Mikoa 26 na hivyo kufikia jumla ya mashine 1,158 ukilinganisha na machine 895 zilizokuwepo kipindi cha mwaka 2022/23.

Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu amesema hayo Bungeni Mei 13, 2024 akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2024/25 na kuelezea utekelezaji wa majukumu ya Wizara katika utoaji wa huduma za Kinga nchini.

“kwa wastani, kila mashine inazalisha tani 30 za unga wa mahindi ulioongezwa virutubishi kwa mwezi hivyo inakadiriwa kiasi cha tani 34,740 zinazalishwa kwa mwezi.” Amesema Waziri Ummy

Amesema, kwa sasa kuna jumla ya viwanda/wasindikaji wakubwa wa vyakula 31 ambapo wazalishaji 9 ni wasindikaji wa unga wa ngano, 13 wa mafuta ya kula na 9 ni wasindikaji wa chumvi ambapo viwanda hivyo vyote vinaongeza virutubishi ili kuimarisha Afya za wananchi.

Aidha, Waziri @ummymwalimu amesema Wizara ya Afya imeendelea na utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa pili wa Kitaifa wa Lishe 2021/22 – 2025/26 kwa afua za lishe zilizothibitishwa kuwa na matokeo makubwa ili kukabiliana na matatizo ya utapiamlo wa lishe duni (Malnutrition) na unene uliokithiri (Obesity).

Waziri Ummy ametaja baadhi ya afua hizo ni pamoja na utoaji wa matone ya vitamin A, dawa za kutibu minyoo ya tumbo, matibabu ya utapiamlo mkali kwa watoto, utoaji wa vidonge vya madini chuma na foliki asidi kwa wajawazito.

“Afua nyingine ni uongezwaji wa virutubishi vya madini na vitamini kwenye vyakula vinavyoliwa kwa wingi ikiwemo unga wa ngano, unga wa mahindi, chumvi, mafuta ya kula, utoaji wa elimu ya lishe na uhamasishaji wa masuala ya ulaji unafoaa kwa kutumia vyakula vinavyopatikana kwenye maeneo yetu pamoja na kufanya mazoezi.” Amesema Waziri Ummy