Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MAKAMPUNI ZAIDI YA 60 YATHIBITISHA KUSHIRIKI MAONESHO YA FAMASIA AFRIKA MASHARIKI, DAR

Posted on: August 25th, 2022Na Mwandishi Wetu, DSM

MAKAMPUNI zaidi ya 60 kutoka nchi mbalimbali duniani, tayari yamethibitisha kushiriki katika maonyesho makubwa ya famasia yanayofahamika kama ‘Pharmatech East Africa’ yatakayofanyika Jijini Dar es Salaam, ukumbi wa Diamond Jubilee, Agosti 30-1 Septemba, mwaka huu.

Hayo yamebainishwa na Rais wa Chama cha Wafamasia nchini [PST], Fadhili Hezekiah wakati wa warsha ya juu ya uelewa wa chama hicho na Waandishi wa Habari, Jijini Dar es Salaam, Ambapo amesema kuwa maandalizi yameshakamilika na hadi sasa tayari makampuni hayo yamethibitisha.

‘’Maonesho haya ni mahususi na muhimu kama Taifa kuweza kujitokeza kujionea kujifunza kwani ni ya kwanza na ya kipekee kwa Tanzania hasa sekta ya afya.

Tunategemea kuwa na makampuni zaidi ya 100, lakini hadi sasa tayari makampuni 60 tayari yamethibitisha hii ni hatua kubwa sana kwetu kama waandaji kwa ushirikiano na kampuni ya ETSIPL.’’ Alisema Rais wa PST, Fadhili Hezekiah.

Aidha, amewaomba wadau na watu mbalimbali ikiwemo Vyuo vya Famasia nchini, kujitokeza kwa wingi kujionea maonesho hayo kwani ni sehemu ambayo watajifunza na kupata mashirikiano.

‘’Maonesho haya yanakuja na vitu mbalimbali. Makampuni yataonesha bidhaa zao ikiwemo dawa, na vifaa tiba, tutaona dawa kuanzia hatu ya awali hadi inapokuja kuwa dawa…kutakuwa na vitu zaidi kutoka kwenye makampuni haya makubwa duniani, ikiwemo Bara la Ulaya, Asia na kwingine,

Tunaomba makundi mbalimbali waje na wajifunze na hata kuona namna ya kuwekeza sekta ya dawa’’ alisema Rais wa PST, Fadhili Hezekiah.

Kwa upade wake, Mtendaji Mkuu wa kampuni ya ETSIPL ya maonesho ya kibiashara kutoka India, Bw. Digvijay Singh ambao wanafanya maonesho hayo kwa kushirikiana na PST, amesema kuwa, Tanzania imekuwa ya bahati kubwa, kwani makampuni makubwa yanakuja kuonesha bidhaa zao ambapo itachagiza fursa za uwekezaji.

‘’Kampuni kubwa kutoka nchi kama India, Uganda, Misri, Kenya, Rwanda na nyingine nyingi Bara la Ulaya, zinakuja kuonesha bidhaa zao, dawa na vifaa tiba, ambapo pia itakuwa ni fursa za wao kuwekeza hapa nchini, hivyo wadau na watu mbali mbali waje waone"