Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADIWANI 60 BUKOBA WAPATIWA MAFUNZO YA KUKABILIANA NA MLIPUKO WA UGONJWA WA MARBURG.

Posted on: April 16th, 2023

Na. WAF Kagera

Madiwani 60 kutoka Halmashauri ya Bukoba Vijijni (41) na Manispaa ya Bukoba (19) wamepata elimu ya ugonjwa wa Marburg na namna ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huo kutoka wa wataalam wa Wizara ya Afya wakishirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI kupitia Mtandao wa Kidini unaoundwa na taasisi nne za kidini -Tanzania Interfaith Partnership (TIP)

Mafunzo hayo yameongozwa na Afisa Habari Mwandamizi kutoka Wizara ya Afya Bw. Said Makora ambaye amewaomba Madiwani hao kuwa mabalozi wazuri wa kuelimisha jamii juu ya ugonjwa wa Marburg na kuendelea kuhamasisha jamii kuendelea kuwa na desturi ya kunawa mikono mara kwa mara pamoja na utoaji wa taarifa mapema pindi mtu anapobainika kuwa na dalili za ugonjwa huo.

“Kazi kubwa ni kuhakikisha mikono inakuwa salama ,madiwani kuweka nguvu panakuwa na miundombinu ya kunawa mikono ,ninyi viongozi ni sehemu kubwa katika kufikisha ujumbe ,ni muhimu kutoa taarifa kwa wakati na kuondoa unyanyapaa” amesema Bw. Makora.

Katika mafunzo hayo Dkt. Emmanuel Mnkeni Kutoka Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma ametoa elimu ya kutambua dalili za ugonjwa wa Marburg na kusema kuwa dalili zinaweza kuonekana kuanzia siku ya 2 hadi siku ya 21 ambazo zinaweza kuambatana na magonjwa mengine kama vile Malaria, homa ambapo pia hupelekea mwili kuishiwa nguvu, macho kuwa mekundu, vidonda vya koo, maumivu ya tumbo.

Katika mafunzo hayo Madiwani wameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na TIP kwa kuwawezesha kupata elimu hiyo na kuahidi kuwa mabalozi wazuri katika kutoa elimu juu ya ugonjwa huo na kuweza kufahamu mapema dalili zake ili kuweza kutoa taarifa kwa wakati.

Kwa upande wake Mratibu wa Tanzania Interfaith Partnership Bw. Livinus Ndibalema amesema kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI wameamua kutoa mafunzo ya ugonjwa wa Marburg kwa kundi muhimu la madiwani kwani wao wana ushawishi mkubwa kupeleka ujumbe katika jamii wanayoiongoza.