MADAKTARI WA MENO NCHINI WATOA UJUMBE KUPINGA VICHOCHEO VYA MAGONJWA YASIYO YA KUAMBUKIZA "NCD's"
Posted on: October 26th, 2026Na Atley Kuni, WAF-Dodoma
Madaktari wa Kinywa na meno waliokutana jijini Dodoma kwa kikao chao cha mwaka wamelazimika kukusanya pipi zilizokuwa zimewekwa kwenye meza zao kama sehemu ya viburudisho, hatua inayotoa ujumbe kuhusu umuhimu wa kupunguza matumizi ya sukari katika kukabiliana na Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (NCDs).
Kikao hicho kinafanyika leo Oktoba 26, 2026 chini ya kauli mbiu “Ubora wa Huduma za Kinywa na Meno ni Wajibu Wangu,” inayosisitiza wajibu wa kila mmoja katika kulinda afya ya kinywa na meno. Tukio hilo limeibua mjadala kuhusu umuhimu wa kuzingatia lishe bora hata katika mikutano na shughuli za kitaalamu.
Akiongea wakati wa Kikao hicho Mratibu wa Afya ya Kinywa na Meno kutoka Wizara ya Afya, Mkurugenzi Msaidizi Dkt. Baraka Nzobo, amesema, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), matumizi makubwa ya sukari huru yanaongeza hatari ya kuoza kwa meno na kuchangia ongezeko la uzito na Magonjwa Yasiyoambukiza.
"WHO inapendekeza sukari huru iwe chini ya asilimia 10 ya nishati yote inayotumiwa kwa siku, huku kupunguza zaidi hadi chini ya asilimia tano kukitajwa kuwa na manufaa ya ziada kiafya" amesema Dkt. Nzobo.
Kitaalamu, sukari inapoliwa, bakteria waliopo kwenye utando wa meno huitumia na kuzalisha asidi inayoshambulia tabaka la nje la jino. Matumizi ya mara kwa mara ya vyakula na vinywaji vyenye sukari yanaweza kuongeza hatari ya meno kuoza, hasa pale usafi wa kinywa unapokuwa hauridhishi.
Nzobo amesema kwa sasa ameendelea na Kampeni hiyo ya kupunguza matumizi ya pipi na vyakula vyenye sukari nyingi kwani ni miongoni mwa hatua zinazoweza kusaidia kuimarisha afya ya kinywa na kupunguza vihatarishi vya magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Dkt. Nzobo amefafanua kuwa, tukio hilo linaongeza mwanga na umuhimu wa taasisi na waandaaji wa vikao kuzingatia viburudisho vyenye afya, kama vile maji ya kunywa na Korosho, badala ya kutegemea vyakula vyenye sukari nyingi.