MADAKTARI BINGWA WAOKOA MAISHA KILOMITA 76 KUTOKA HOSPITALI YA WILAYA
Posted on: May 16th, 2024
Na WAF, Manyoni- Singida
Ujio wa Madaktari Bingwa wa Rais Samia katika wilaya ya Manyoni umeweza kusaidia kuokoa Maisha ya mama na mtoto aliefuatwa Kilomita 76 kutoka katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni.
Hayo yamebainishwa na Dkt. Halima Basila Daktari bingwa wa Afya ya Uzazi, Mama na Magonjwa ya Wanawake, ambapo alipata taarifa majira ya saa 5 usiku na kumlazimu kumfuata mgonjwa huyo kilomita 76 kutoka katika Wilaya ya Manyoni na kufanikiwa kuokoa maisha ya mama na mtoto.
Dkt. Halima ameeleza kuwa katika kipindi cha hicho za ujio wao katika wilaya hiyo, wamefanikiwa kutoa huduma za kibingwa zilizosaidia kuzuia vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua huku akisema kuwa juhudi hizo zimechangia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha afya ya uzazi na kupunguza vifo vinavyoweza kuepukika.
"Ujio wetu umesaidia kuokoa maisha ya mama na mtoto katika Wilaya ya Manyoni, tumejitahidi kutoa huduma za kibingwa na ushauri nasaha kwa wanawake wajawazito, na tunafurahi kuona matokeo mazuri." Amesema Dkt. Halima.
Aidha, ameelezea nia yao ya kuendelea kufanya kazi kwa karibu na jamii na watoa huduma za afya kupitia kampeni hizo ili kuhakikisha kila mama na mtoto wanapata huduma bora za afya wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua.
Kwa upande wake Magdalena Njinje mkazi wa Ngongo amewashukuru madaktari hao kwa kujitoa na kuweza kunusuru Maisha yake kwani wakati akiwa anapatiwa matibabu hakuwa akijitambua.
Hata hivyo, Wananchi wa Manyoni wamepokea ujio wa Madaktari bingwa wa Rais Samia kwa shangwe na furaha, wakiishukuru serikali kwa kuleta huduma za kibingwa karibu na makazi yao.
Mwisho.