MADAKTARI BINGWA WA SAMIA WAPELEKA KICHEKO HOSPITALI YA WILAYA YA PANGANI
Posted on: May 23rd, 2024
Na WAF - Pangani
Jopo la Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia waliokita kambi kwenye Hospitali ya Wilaya ya Pangani tangu siku ya Jumanne tarehe 21 Mei, 2024 wamekua chachu ya furaha kwa watumishi wa Hospitali hiyo pamoja na wananchi baada kusaidia kupatikana mashine ya kisasa ya usingizi salama ambayo haikuwepo toka Hospitali hiyo ianzishwe.
Dkt. Athuman Kihara ambaye ni kiongozi wa kambi hiyo amesema hayo jana tarehe 23 Mei 2024 wakati akitoa taarifa ya mwenendo wa kambi toka walipofika kuanza kutoa huduma.
“Tangu tumefika hapa tulikuwa na changamoto ya mashine ya usingizi ambayo haikuwepo kwahiyo kupitia Mganga Mfawidhi wa Hospitali hii pamoja na Viongozi wengine wa Serikali ambao walifanikisha upatikanaji wa mashine hiyo kufika jana ambapo Daktari wetu wa usingizi amesaidia kuihuisha na rasmi imeanza kufanya kazi na kusaidia kurahisisha utoaji wa matibabu hasa ya upasuaji kwa wakazi wa Wilaya ya Pangani”. Amesema Dkt. Athuman.
Kufuatia kupatikana kwa mashine pamoja na kujengewa uelewa watumishi jinsi ya kuitumia hivi sasa Hospitali inweza kufanya upasuaji mkubwa na mdogo kitu ambacho awali haikuweza kufanyika bali wagonjwa walikua wanapewa rufaa ya kwenda hospitali nyingine.
Kambi hiyo yenye jumla ya Wataalam watano katika kada za Magonjwa ya wanawake na Uzazi, Usingizi salama, Magonjwa ya watoto, Magonjwa ya ndani pamoja na upasuaji wamepongeza wananchi wa wilaya ya Pangani kwa kujitokeza hospitalini hapo kuja kupatiwa matibabu tangu kambi hiyo ilipoanza.
Aidha, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Hassan Msafiri ameshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha Madaktari kuleta kambi hizo katika ngazi ya msingi kwa kuwaongezea ujuzi kwa mafunzo mbalimbali.