Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADAKTARI BINGWA WA SAMIA WAOMBWA KUBORESHA HUDUMA VITUONI

Posted on: September 23rd, 2024

Na WAF - SINGIDA

Timu ya Madaktari bingwa wa Rais Samia iliyoko Mkoani Singida imeombwa kwenda kuimarisha huduma kwa kutoa ujuzi kwa watumishi walioko katika vituo wanavyoenda ili kuwasaidia kuwa na weledi na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Wito huo umetolewa leo tarehe 23 Septemba, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendengo wakati akiwapokea Madaktari Bingwa hao takribani 42 ambao watatoa huduma katika Halmashauri saba zinazopatikana Mkoani humo.

"Mbali na kwenda kutoa huduma kwa mtu mmoja mmoja lakini pia nendeni mkaimarishe timu zetu ziweze kufanya kwa weledi pamoja kupata ujuzi ikiwa lengo letu ni kuokoa uhai wa watu ambao wanaweza kupata tiba za kibingwa". Amesema Mhe. Halima.

Aidha, Mkuu wa Mkoa huo ametoa rai kwa wanachi wote wa Halmashauri ambazo Madaktari hao wataenda kujitokeza kwa wingi kupata huduma za kibingwa ikiwemo kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali pamoja na kupewa huduma za matibabu zinazostahili ikiwemo kufanyiwa upasuaji.

Madaktari bingwa hao wataweka kambi ya siku saba katika Halmashauri zote za Mkoa wa Singida huku wakiahidi kutoa huduma ambazo hapo awali wananchi walikua wanasafiri umbali mrefu kuzifuata.