Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADAKTARI BINGWA WA SAMIA WAMREJESHEA FURAHA MTOTO JACKLINE , SINGIDA

Posted on: May 17th, 2024



Na WAF, Singida

Madaktari Bingwa na Bobezi wa Samia wakiwa mkoani Singida wamefanikisha upasuaji mkubwa kwa mtoto mwenye umri wa miaka mitatu aitwaye Jackline Wilson mkoani humo, na kumtolea uvimbe aliodumu nao kwa muda miaka mitatu

Akizungumza mara baada ya upasuaji huo Daktari bingwa wa Upasuaji Nassib Msuya amesema upasuaji huo ambao umefanyika katika Hospitali ya Manispaa Singida umefanyika kwa ushirikiano wa madaktari walioweka kambi katika Hospitali hiyo.

"Mtoto Jackline Wilson, amekuwa akisumbuliwa na uvimbe huu kwa muda mrefu, hali hali iliyosababisha ashindwe kushiriki kwenye majukumu ya utoto ikiwepo kucheza na wenzake" amesema Dkt. Msuya

Kwa upande wake Daktari bingwa wa ganzi na usingizi Dkt. Anna Doho amesema kuwa operesheni hiyo ilikwenda vizuri na wanatarajia mtoto huyo kupona kabisa bila matatizo yoyote ya kiafya huku akiongezea kuwa kufanikisha upasuaji huo ni ushahidi wa maendeleo makubwa katika sekta ya afya nchini, hasa katika maeneo ya vijijini ambako huduma za upasuaji zimekuwa adimu.

Akiongea mara baada ya upasuaji huo, mzazi wa Mtoto Jaqline aitwaye Pendo Said, aliyeshindwa kuzuia hisia zake ametoa shukrani zake za dhati kwa Rais Samia na timu ya madaktari bingwa kwa jitihada zao kubwa na matibabu waliopokea.

"Tumepokea matibabu haya mkubwa kutoka kwa madaktari hawa, hatuna neno la kutosha kueleza furaha yetu. Mtoto wetu sasa ataweza kukua vizuri katika makuzi yake, amesema mama wa mtoto Bi Pendo.

Kampeni Kabambe ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia inaendelea kuleta matumaini kwa familia nyingi nchini Tanzania, ikionyesha jinsi serikali inavyojitoa kwa dhati kuboresha maisha ya wananchi wake kupitia huduma bora za afya.

MWISHO