Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADAKTARI BINGWA WA SAMIA KUPUNGUZA GHARAMA ZA MATIBABU YA KIBINGWA MKOANI KATAVI

Posted on: June 10th, 2024Na WAF - Katavi

Ujio wa Madaktari Bingwa wa Rais Samia katika mkoa wa Katavi utasaidia wananchi kupata huduma za kibingwa kwa gharama nafuu katika hospitali za wilaya zao hivyo wananchi wa Katavi wajitokeze kwa wingi kufika katika hospitali zao za wilaya waweze kupatiwa matibabu ya Kibingwa

Hayo yamesemwa na Mganga mkuu wa Mkoa wa Katavi Dkt. Jonathan Budenu katika mapokezi ya Madaktari Bingwa 25 wa fani mbalimbali za kibingwa ambao watatoa huduma katika halmashauri zote 5 za mkoa wa Katavi kuanzia Tarehe 10 Juni, 2024 mpaka 14 Juni, 2024.

Dkt. Budenu amesema mkoa wa Katavi una Madaktari Bingwa wachache hivyo kwa kuletwa madaktari hawa kwenda katika halmashauri zote itasaidia kuwapunguzia wananchi gharama ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo Katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa nje ya mkoa.

“Katika mkoa wetu kuna baadhi ya halmashauri zipo umbali zaidi ya kilomita 150 ambao kuja katika ngazi ya mkoa kupata huduma inakuwa ngumu na gharama kubwa, kwa madaktari hawa kufika katika maeneo hayo zitawasaidia wananchi ambao uwezo wao ni mdogo kuweza kupata matibabu ya kibingwa” Amesema Dkt. Budenu.

Pia Dkt. Budeno amesema Madaktari hawa pamoja na kutibu wagonjwa mbalimbali pia watawajengea uwezo madaktari waliopo katika ngazi za halmashauri ili ujuzi huo watakao pata uwe endelevu katika kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Watakapo ondoka madaktari hawa watakuwa wamewajengea uwezo, hata kama watakuwa sio madaktari bingwa watakuwa wamepata ujuzi kazini na kuona ni jinsi gani watakuwa wakiendelea kutumia ujuzi huo”.

Akiongea kwaniaba ya Madaktari bingwa Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura Dkt. Manyasani Gisoli amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kuweza kupata huduma za kibingwa kwa gharama nafuu katika hospitali za Wilaya zao.

“Tumekuja kutoa huduma za Kibingwa kuna madaktari Bingwa wa Watoto, Magonjwa ya Dharura, Magonjwa ya kina mama, Upasuaji na Magonjwa ya ndani tunaomba wananchi wajitokeze kwa wingi ili kufaidika na huduma hizi”Amesema.

MWISHO.