MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA WAWE CHACHU KWA AFYA ZA WANA MBEYA
Posted on: October 30th, 2024Na WAF, MBEYA
Wananchi mkoani mbeya wametakiwa kuchangamkia fursa ya ujio wa Madaktari Bingwa na Bobezi wa Rais Samia mkoani hapa kwa ajili yakupata suluhu ya changamoto za Afya.
Pia Madaktari Bingwa wa Rais wametakiwa kuwajengea uwezo watoa huduma za afya kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa Halmashauri zote za mkoa huo wa Mbeya kwa siku zote sita watakazoweka kambi.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera leo, Septemba 23, 2024, wakati akiwapokea na kuzindua kambi ya matibabu ya madaktari Bingwa wa Rais Samia, iliyowekwa katika Mkoa huo kuanzia Septemba 30 hadi Oktoba 05, 2024.
"Mkoa wetu umepokea jumla ya madaktari Bingwa na Bobezi 50 ambapo kila halmashauri imepata madaktari bingwa sita na muuguzi mbobezi 1, isipokuwa Halmashauri ya Mbeya Jiji, ambayo itakuwa na madaktari bingwa saba ambao watafanya kazi kwa siku sita, ni wajibu wa wananchi wetu kuchangamkia fursa hii adhimu" amesema RC Homera.
Mhe. Homera amesema kampeni ya awamu ya kwanza walifanikiwa kuwafikia wananchi wapatao 2,859 kwa huduma mbalimbali, ikiwemo huduma za magonjwa ya ndani, upasuaji, watoto, wachanga, na huduma za usingizi na ganzi.
Amefafanua kuwa Jumla ya watoa huduma 307 walijengewa uwezo katika maeneo ya kazi huku mapato yakiongezeka kwa kukusanya kiasi cha fedha 53,063,654/= kilikusanywa katika kipindi cha kampeni siku za kampeni.
“Ni matarajio yetu kuwa baada ya siku sita za uwepo wenu katika hospitali zetu za halmashauri, Mkoa utaendelea kuboresha huduma za wagonjwa wa nje na wa ndani wenye magonjwa mbalimbali, na kuimarisha huduma za watoto wachanga katika ngazi ya halmashauri, hali itakayopunguza rufaa.”amesema Mhe. Homera
Serikali inaendelea kutoa kipaumbele kwenye sekta ya afya, hususan ni kuwasogezea wananchi huduma za kibingwa katika hospitali za halmashauri, ikiwa na lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi wenye shida za kiafya.